Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linawasaka watu watano wanaodaiwa
kuwa ni majambazi ambao walivamia duka la Mfanyabiashara mmoja anayefahamika
kwa jina la Msafiri Tullo (40) mkazi wa mji mdogo wa Kigonsera wilayani Mbinga
mkoani humo na kumpora fedha taslimu za mauzo shillingi milioni 15,250,000
pamoja na simu mbili za kiganjani aina ya Tecno, zenye thamani ya shilingi
110,000 na kutokomea kusikojulikana.
Zubery Mwombeji. |
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Ofisini kwake
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo
lilitokea juzi majira ya saa 1:30 jioni katika mji huo wa kigonsera.
Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo palitokea kundi
la watu watano huku wakiwa na silaha za jadi ambazo walikuwa wameshika mkononi,
ambapo walipowasili dukani hapo walianza kumshambulia Msafiri kwa kumpiga
sehemu mbalimbali za mwili wake na kufanikiwa kumpora fedha hizo huku
wakimjeruhi sikio lake la upande wa kushoto na muuzaji wake wa duka hilo,
Melkion Nchimbi (18).
Alisema kuwa majambazi hao walikuwa na silaha za jadi virungu
na mapanga ambapo baada ya kupora fedha hizo waliondoka huku wakikimbia na
kuelekea kusikojulikana na kwamba Majeruhi hao, walikimbizwa katika kituo cha
afya Kigonsera ambacho ni cha Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga ambako walipatiwa
matibabu na kuruhusiwa kurudi makwao.
Kamanda Mwombeji alieleza kuwa Polisi mkoani Ruvuma, hivi
sasa inawasaka watuhumiwa hao ambao wanadaiwa kukimbilia kwenda Songea mjini na
pale watakapofanikiwa kuwakamata watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment