Na Kassian Nyandindi,
Tunduru.
HOSPITALI kongwe ya Misheni Mbesa ambayo inamilikiwa na Kanisa la
Bibilia Tanzania wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ipo katika hali mbaya yenye
kuhatarisha kufungwa wakati wowote kuanzia sasa kutokana na Madaktari kutoka
nje ya nchi ambao walikuwa ni tegemeo kubwa katika kuendesha hospitali hiyo kuanza
kufunga virago kurejea makwao, baada ya mikataba yao ya kufanya kazi kwisha.
Hospitali ya Misheni Mbesa. |
Katibu tawala wa hospitali hiyo, Dkt. John Mwaya alisema hayo
wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya hospitali yake kwa Mkuu wa
wilaya ya Tunduru, Juma Homera ambaye alifanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo
kwa lengo la kujionea maendeleo mbalimbali.
Dkt. Mwaya alibainisha kuwa changamoto kubwa inayotishia kufa
kwa hospitali yake ni kuwepo kwa upungufu wa Madaktari wenye taaluma na wauguzi
walio somea fani hiyo ili kuweza kutosheleza ikama husika.
Alisema kuwa hospitali ya Mbesa ambayo ni tegemeo kubwa kwa
wananchi waishio wilayani Tunduru na nje ya wilaya hiyo tangu mwaka 1957 kuna
kila sababu kwa serikali, kuchukua jitihada za makusudi katika kuinusuru kwa
kupeleka wataalamu wa fani za kitabibu pamoja na kuipunguzia mzigo wa kuwalipa
mishahara baadhi ya watumishi wenye sifa watakaohudumia hospitalini hapo.
Naye Kaimu Mkuu wa shirika la Misheni Mbesa, Heiga Armbruster
alipongeza ujio wa Mkuu wa wilaya hiyo na kueleza kuwa anayoimani kwamba kero
hizo zitatatuliwa na kuifanya hospitali iweze kuendelea kutoa huduma kwa
wagonjwa wanaohitaji matibabu.
Akijibu kero hizo Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera
aliwataka viongozi wa hospitali hiyo kuorodhesha changamoto zinazowakabili na
kuzipeleka haraka Ofisini kwake, ili aweze kuwasiliana na Waziri mwenye dhamana
kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment