Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amepiga marufuku unywaji pombe
saa za kazi na kumtaka Afisa biashara mwenye dhamana ya kusimamia suala hilo,
ahakikishe kwamba anadhibiti hali hiyo ili isiweze kuendelea katika maeneo
mbalimbali wilayani humo.
Nshenye
alitoa rai hiyo juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji
wa Mbinga, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa ambapo
aliagiza pia kuwashughulikia wale wote ambao wanauza pombe saa za kazi asubuhi.
“Leseni za
biashara naagiza zinyang’anywe kwa wale wanaouza pombe saa za asubuhi, haiwezekani
watu wanaacha kufanya kazi badala yake utaona wanakwenda kwenye baa na kunywa
pombe, pombe zote zianze kunyweka kuanzia saa tisa jioni”, alisisitiza Nshenye.
Aliongeza
kuwa kwa wale watumishi ambao watashindwa kusimamia majukumu ya kazi zao
ipasavyo, wajiandae kuacha kazi au wajiondoe mapema wenyewe kabla
hawajachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi.
Mkuu huyo wa
wilaya alisema kuwa muda wa mtumishi kufanya kazi kwa mazoea umepita, hivyo ni
wakati wa kutimiza majukumu ya kazi zao ili jamii iweze kunufaika na huduma
zinazotolewa na serikali.
Kadhalika
kupitia baraza hilo la Madiwani, Nshenye alitoa agizo kwa kuwataka pia wananchi
wale wote wanaosha magari kwenye vyanzo vya maji waondoke mara moja katika
maeneo hayo kwani huo ni uharibifu na uchafuzi wa mazingira.
“Ninatoa
agizo kwa Afisa mazingira asimamie hili kwa sababu ndio wajibu wake, kamata
gari lolote lile linalooshwa mtoni lipelekwe ofisi za halmashauri lipigwe
faini, tusigombane na waosha magari tugombane na wamiliki wa magari”, alisema.
Mwenyekiti wa
halmashauri ya mji wa Mbinga, Ndunguru Kipwele kwa upande wake alimhakikishia
Mkuu huyo wa wilaya kwamba maagizo hayo aliyoyatoa atahakikisha anayasimamia
ipasavyo na kufanyiwa utekelezaji ili yaweze kuzaa
matunda.
No comments:
Post a Comment