Na Muhidin Amri,
Songea.
SERIKALI mkoani Ruvuma, imepiga marufuku upigaji picha
kwa wagonjwa wanaolazwa wodini au katika vituo mbalimbali vya kutolea
huduma za afya katika mkoa huo.
Onyo hilo limetolewa hivi karibuni mjini Songea na Mganga
mkuu wa mkoa huo, Dkt. Damas Kayera kwa niaba ya Katibu tawala wa mkoa huo, Hassan
Bendeyeko.
Dkt. Damas Kayera. |
“Kuanzia sasa ni marufuku vitendo vya upigaji
picha wodini kwa kutumia kamera au vifaa vyovyote vyenye uwezo
wa kupiga picha kama vile simu za mkononi", alisema Dkt.
Kayera.
Alisema kuwa wamepiga marufuku kutokana na kile walichobaini kuwa
vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya ndani ya mkoa huo, kumekuwa na
tabia kwa baadhi ya wananchi kupiga picha wodini pale wanapokuja kuwajulia hali
ndugu zao waliolazwa bila kibali maalumu.
Dkt. Kayera alisema kuwa vitendo hivyo vinafanywa ama kwa
lengo zuri la kuwajulisha jamaa zao hali ya mgonjwa wao au kwa malengo ambayo
sio mazuri ambapo baadhi ya picha zimekuwa zikioneshwa kwenye mitandao ya
kijamii zikiwa na ujumbe wa kupotosha.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na watoto katika barua yake kwa makatibu tawala wa mikoa Tanzania bara,
inaeleza kuwa Wizara imetoa tamko la kukataza kupiga picha wodini kwa kuwa
inasimamia viwango na miiko ya utoaji huduma za afya.
Waganga wakuu wa mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri zote
nchini wanatakiwa kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kwamba wananchi
wanatakiwa kuelimishwa umuhimu wa kuwasilisha malalamiko yao pale
inapotokea ukiukwaji wowote katika utoaji wa huduma za afya.
Katika hatua nyingine Manispaa ya Songera nayo imeanza
kutekeleza agizo la kupiga marufuku upigaji picha wodini kwenye vituo vyote vya
kutolea huduma za afya katika Manispaa hiyo.
Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa tayari Mkurugenzi
mtendaji wa Manispaa hiyo ametoa maagizo kwa Mganga mkuu wa Manispaa ya Songea
kuhakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa kwa vitendo katika hospitali na vituo
vya afya.
No comments:
Post a Comment