Na Julius Konala,
Tunduru.
MBUNGE wa Jimbo la Tunduru kusini mkoani Ruvuma, Daimu
Mpakate ametoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya shilingi
milioni 100 ili viweze kutumiwa na wananchi wake jimboni humo, kwa ajili ya
kuwaletea maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Daimu Mpakate. |
Kwa mujibu wa Mbunge huyo alisema kuwa miongoni mwa misaada
iliyotolewa ni mashine nane za kusaga nafaka zenye thamani ya shilingi milioni
16, vitabu vya kiada na ziada kwa shule za sekondari vyenye thamani ya shilingi
milioni 32, mashine za kushonea nguo (vyerehani) nane vyenye thamani ya shilingi
milioni 2, pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 2 kwa ajili ya kugharimia
kushona sare za shule kwa wanafunzi 120 watakaochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato
cha kwanza mwakani.
Mpakate alitoa msaada huo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye viwanja vya serikali ya kijiji cha Mbesa wilayani humo ambapo vifaa
hivyo vilitolewa kwa matumizi ya jamii kupitia shule nane za sekondari ambazo
ni Nalasi, Mbesa, Mchoteka, Malumba, Ligoma, Lukumbule, Namasakata na Semeni.
Vifaa vingine vilivyokabidhiwa katika mkutano huo ni pamoja
na magodoro 30 yenye thamani ya shilingi milioni 2.1 kwa ajili ya kuwasaidia
wauguzaji wa wagonjwa ambao hulazwa katika hospitali ya Misheni Mbesa ambao
hapo awali walikuwa wakilala chini.
Mbunge huyo aliongeza kuwa katika bajeti yake, ametenga pia jumla
ya shilingi milioni 80 ambazo zitatoka katika mshahara wake kwa lengo la kuwasaidia
na kuwahudumia wananchi wa jimbo la Tunduru kusini.
Naye Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera pamoja na
kumpongeza kwa juhudi anazozifanya Mbunge huyo alisema kuwa wapo wabunge wengi
ambao wanaouwezo wa kusaidia wananchi wao, lakini wamekuwa hawawezi kujitoa kwa
moyo katika kuchangia shughuli za maendeleo kwenye majimbo yao.
“Wakati wa kampeni baadhi ya wabunge wamekuwa wakitoa ahadi
nyingi kwa wananchi wao, lakini baada ya kushinda tu chaguzi zilizopita matokeo
yake huwa ni kinyume kutokana na wengi wao kushindwa kutimiza ahadi walizotoa
kwa wananchi wao”, alisema Homera.
No comments:
Post a Comment