Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
ASKOFU wa Kanisa katoliki jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John
Ndimbo ameitaka serikali ya awamu ya tano kutokuwa na huruma kwa wanaume ambao
wanakatisha masomo ya wanafunzi wa kike waliopo mashuleni kwa kuwapa mimba huku
wengine wakidiriki kuwaoa, kwani ni wakati sasa wa kuwachukulia hatua na adhabu
kali za kisheria ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Askofu John Ndimbo. |
Askofu Ndimbo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa
akizungumza na madiwani, watumishi na baadhi ya wananchi waliohudhuria kikao
cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga kilichoketi kwenye ukumbi
wa Umati uliopo mjini hapa.
Alieleza kuwa baadhi ya wanaume tena wenye umri mkubwa, wakiwemo
walimu na watumishi wengine wa serikali wamekuwa na tabia mbaya ya kufanya
mapenzi na watoto hao ambao bado wanaendelea na masomo shuleni jambo ambalo
limekuwa likikatisha ndoto zao na matumaini ya wasichana wengi, katika maendeleo
yao ya sasa na baadaye.
Pamoja na mambo mengine Askofu huyo ameishauri serikali
kupitia halmashauri za wilaya, kuiangalia kwa jicho la huruma shule ya
msingi Kitulo iliyopo wilayani hapa ambayo ina hali mbaya ambapo kuta zake zimejenga
nyufa, kupasuka kwa milango, madirisha na walimu kukosa hata sehemu ya ofisi yenye
hadhi ambayo inaweza kuwafanya wafanye kazi kwa moyo wa kujituma.
Sambamba na hilo Askofu Ndimbo alibainisha kuwa ni muhimu sasa
kwa serikali kufanya upendeleo wa kutenga kiasi cha fedha ili kuifanyia ukarabati
shule hiyo ambapo hata walimu wake, wameonekana kukata tamaa kutokana na hali
mbaya ilivyo jambo ambalo linawafanya washindwe kutekeleza wajibu wao
kikamilifu na kurudisha nyuma kiwango cha taaluma.
Kadhalika amewataka Madiwani wa wilaya ya Mbinga kuendeleza umoja
wao kwa kujenga ushirikiano na kuvumiliana kwa kufanya kazi pamoja kama mchwa
na kuweka kando tofauti zao za vyama vya kisiasa.
Mbali na pongezi hizo pia Askofu Ndimbo alisisitiza kuwa ni
wakati sasa wa kuwa makini katika usimamizi na ufuatiliaji wa fedha
zinazotengwa kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii katika kata zao, ikiwemo
kuwashirikisha wananchi wao na kuwahimiza kujenga ushirikiano katika kuibua na
kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment