Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amesema kwamba asilimia 80 ya kahawa inayozalishwa wilayani humo Wakulima wake hawauzi
wao wenyewe katika minada ya kuuzia zao hilo, bali imekuwa ikiuzwa na Walanguzi
hivyo serikali itaendelea na msako mkali wa kuwakamata watu wanaotumia mbinu
hizo za ujanja kuwarubuni wakulima.
Cosmas Nshenye. |
Nshenye alisema hayo juzi alipokuwa akitoa salamu za serikali
kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, ambapo
alieleza kuwa katika msimu wa uzalishaji kahawa mwaka huu makampuni kadhaa
yalikamatwa na kupigwa faini baada ya kukiuka taratibu na sheria zilizowekwa
juu ya manunuzi ya zao hilo.
Aidha alisisitiza juu ya makampuni hayo kuhakikisha kwamba
yanalipa malipo ya ya pili ya mkulima na kuachana na biashara haramu ya magoma
ambayo humnyonya mkulima na kumfanya aendelee kubaki kuwa maskini.
“Nawataka viongozi wenzangu tuendelee kusimamia hili ili
wakulima wetu waweze kulipwa malipo ya pili, sisi tumepewa dhamana na serikali
kwa ajili ya kuwatumikia watu”, alisema Nshenye.
Pia aliongeza kuwa sheria ndogo zilizotungwa katika kumsaidia
mkulima namna ya kupambana na biashara ya magoma ya kahawa, inatakiwa iendelee
kufanya kazi kwa kumsaidia mkulima ili aweze kuwa na kipato kitakachomsaidia
kuweza kupata fedha za kununua hata pembejeo za kilimo ambazo ataweza
kuendeleza mazao yake shambani.
“Sisi kama halmashauri tumetunga sheria ndogo ambazo sasa
tunapaswa kuzisimamia na kumfanya mkulima huyu aweze kunufaika nazo, wewe ukiwa
afisa kilimo timiza majukumu yako ya kazi ni aibu kuona kiongozi wa serikali
unakuwa wa kwanza kumkandamiza mkulima, atakayebainika atachukuliwa hatua za
kisheria”, alisisitiza.
Hata hivyo akizungumza kwa niaba ya Madiwani wenzake
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Ambrose Mtarazaki alimhakikishia
Mkuu wa wilaya hiyo, Nshenye kwamba wataendelea kushirikiana kwa pamoja katika
kudhibiti matatizo yanayowakabili wakulima ikiwemo tatizo hili la biashara
haramu ya magoma ya kahawa ambalo limekuwa likimtesa mkulima na kumfanya
aendelee kubaki kuwa maskini.
No comments:
Post a Comment