Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya Watumishi wa serikali waliopo katika halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamelalamikiwa wakidaiwa kutumia muda mwingi
kufanya biashara haramu ya magoma ya kahawa licha ya serikali kukemea vitendo
hivyo kwa muda mrefu ikiwataka waache mara moja.
Aidha wamenyoshewa kidole kwamba kwa kuwa ndiyo wamekuwa
vinara namba moja kufanya biashara hiyo kwa lengo la kumdhulumu mkulima
anayezalisha zao hilo, kwa atakayekamatwa atapewa adhabu kali ikiwemo
kufikishwa mahakamani ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama
hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye alimweleza hayo Mkuu
wa mkoa huo Dkt. Binilith Mahenge wakati alipokuwa amewasili wilayani hapa
katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo
wilayani humo.
Nshenye alimweleza Dkt. Mahenge kuwa pamoja na serikali
kupiga marufuku biashara hiyo bado kuna watumishi wachache wa umma, wamekuwa
wakiendelea kuifanya na kwamba serikali imeweka mitego yake ili kuweza
kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Tatizo kubwa hapa washiriki ni viongozi wenyewe wa serikali
kutoka ndani ya halmashauri, nimetoa maagizo kwa kamati yangu ya ulinzi na
usalama kushughulikia tatizo hili kwa nguvu zote”, alisema Nshenye.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge amemtaka
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga kusimamia ipasavyo sheria zilizopo juu ya namna
ya kudhibiti biashara hiyo ya magoma ya kahawa ili mkulima asiweze kuibiwa
kahawa yake.
Dkt. Mahenge alisisitiza kuwa kwa mtu yeyote atakayematwa awe
ni mtumishi wa serikali au la, afilisiwe kahawa aliyokamatwa nayo na kupigwa
faini sambamba na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kukiuka taratibu na sheria
zilizowekwa na serikali.
No comments:
Post a Comment