Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Luckness Amlima ameipongeza
asasi isiyokuwa ya serikali ya Huruma iliyopo wilayani hapa kwa kutoa msaada wa
nguo kwa watoto yatima 308 ambao wanaishi katika mazingira magumu, ambazo hutoka
katika kata ya Rwinga na Namtumbo mjini hapa.
Pongezi hizo alizitoa wakati alipokuwa akizungumza juzi na
wananchi mjini Namtumbo, wakati wa zoezi la ugawaji wa nguo hizo za watoto hao zilizotolewa
na Shirika la Japan Relief Center (JRC) kutoka nchini Japan kupitia asasi hiyo.
Amlima alisema kuwa kuna kila sababu kwa asasi nyingine
zilizopo ndani na nje ya wilaya hiyo, kuiga mfano kama huo wa kusaidia watoto
hao kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu ili waweze kuondokana na dhana ya
kujisikia kama vile wametengwa.
Naye Mkurugenzi wa asasi ya Huruma, Asumpta Ndauka aliwataka
wazazi wilayani Namtumbo kuwalea watoto hao kikamilifu na kuacha tabia ya
kuwatenga au kuwanyanyasa kwa namna moja au nyingine.
Kwa upande wake mtoto Ashura Mohamed (10) aliushukuru uongozi
wa asasi hiyo kwa kuwaletea nguo hizo ambapo alisema kuwa, zitaweza kuwafanya
waweze kuvaa na kupendeza kama walivyo watoto wengine.
Shirika la Huruma ni asasi isiyokuwa ya serikali ambayo
hujishughulisha na kuhudumia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira
magumu, wajane, kutoa elimu juu ya kuepukana na maambukizi ya Virusi vya
ukimwi na utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment