Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAKAZI waishio katika kijiji cha Matetereka katika kata ya
Matetereka Jimbo la Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameuomba uongozi wa
mkoa huo kuingilia kati na kumchukulia hatua Mwenyekiti wa kijiji hicho, Remigius
Njafula ambaye anatuhumiwa kuwalinda kwa kuwakumbatia baadhi ya wananchi wanaolalamikiwa
kuweka sumu katika chanzo cha maji kinachotumiwa na wananchi hao.
Mkuu wa mkoa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge. |
Aidha kufuatia tukio hilo wameuomba pia uongozi huo wa mkoa kuwasaidia
kumwondoa madarakani Mwenyekiti huyo, kutokana na kitendo hicho cha kuwabeba
watu wanaotuhumiwa kuweka sumu aina ya Round up ambayo inatumiwa kuulia magugu
shambani.
Tukio hilo hivi sasa limesababisha kwenye chanzo hicho cha
maji kijijini Matetereka, kaya zaidi ya 50 kukosa huduma ya maji safi na salama, kutokana na
kuhofia endapo wakiendelea kuyatumia maji hayo huenda wakaathirika afya zao.
Licha ya tuhuma hiyo kuendelea kumtafuna Mwenyekiti huyo, pia
analalamikiwa kwamba yeye pamoja na kamati yake ya maji wanadaiwa kula fedha za
mchango ujenzi wa mradi wa maji shilingi milioni 21, ambazo zilichangwa na
wananchi pamoja na wadau mbalimbali.
Njafula ananyoshewa kidole kwa kutosoma mapato na matumizi ya
kijiji kwa muda mrefu sasa na kutumia madaraka yake vibaya, kwa kuwagawia
vipande vya ardhi baadhi ya marafiki zake kijijini humo bila kufuata taratibu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti Mwenyekiti
wa kikundi cha maji kijiji cha Matetereka, Fedrick Njarika alisema kuwa
wanashindwa kusonga mbele kimaendeleo katika kuufanya mradi huo wa maji uwe
endelevu kutokana na vikwazo vinavyojitokeza ambavyo vinasababishwa na
Mwenyekiti huyo ambaye bado yupo madarakani.
“Hata katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana,
Mbunge wetu Joseph Mhagama aliahidi kutuchangia kiasi cha shilingi milioni nane
ili kuweza kufanikisha kukamilisha ujenzi wa mradi huu, ahadi ambayo
ameitekeleza kwa kutoa milioni tisa lakini hadi sasa Mwenyekiti wa kijiji hiki
hataki kutoa taarifa ya kupatikana kwa fedha hizi kwa wananchi wake”, alisema
Njarika.
Aliongeza kuwa katika chanzo hicho ambacho kinategemewa kwa
ajili ya kulisha maji wananchi wa kijiji cha Matetereka, hivi sasa kina hali
mbaya kwani hata makopo na vizibo vya dawa hiyo ya kukaushia magugu yametupwa
katika eneo la chanzo hicho.
Naye Benjamin Luambati ambaye ni Ofisa mtendaji wa kijiji
hicho alisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya wahusika waliofanya uhalifu
huo, ili wananchi wasiweze kuathirika dhidi ya sumu ya dawa inayodaiwa kuwekwa
kwenye maji hayo ambayo yalikuwa yakitumiwa na wakazi hao.
Vilevile Moses Njalika ambaye ni mkazi wa kijiji cha
Matetereka alisema kuwa pamoja na ufuatiliaji kufanyika juu ya matumizi mabaya
ya fedha hizo zilizochangwa na wananchi, hali inaonesha kuwa baadhi ya pesa
wamekopeshana viongozi wa kijiji kinyume na taratibu ndiyo maana mradi huo
unashindwa kukamilika ujenzi wake.
Naye Mchungaji wa Kanisa la EAGT kijijini hapo, Steven Mtema
alieleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona watu walioweka sumu katika chanzo
hicho wanaendelea kulindwa hivyo ni vyema serikali iwachukulie hatua za
kisheria ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia mbaya kama hiyo.
“Binafsi naona kama hatupo salama, kwani nimeumizwa sana na
vitendo vya ubabe na vitisho tunavyofanyiwa hapa kijijini kwetu mtu anavunja
sheria kwa kulima kwenye vyanzo vya maji, huku akipuliza madawa ambayo ni sumu
kwa binadamu na bado analindwa kwa maslahi ya Mwenyekiti baadhi tukihoji
tunaonekana kuwa ni wakorofi”, alisema Mchungaji Mtema.
Alipotafutwa na mwandishi wetu ili aweze kutolea ufafanuzi
juu ya madai hayo Mwenyekiti wa kijiji cha Matetereka, Njafula alionesha ukali
na kugeuka kuwa mbogo huku akimweleza mwandishi wa habari hizi kwamba haogopi
kitu chochote na hakuna kiongozi yeyote wa ngazi ya wilaya au mkoa atakayeweza
kumchukulia hatua dhidi yake.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kwamba taarifa
za matukio ya kijiji hicho Ofisi yake imezipata na kuahidi kwenda kufanya haraka
mkutano na wananchi hao, ili kuweza kutatua kero hiyo mapema kabla madhara
hayajatokea na kuathiri jamii.
“Hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria, watakaotuhumiwa wote na wale ambao wamelima kwenye vyanzo vya maji pale kijijini na kuweka hiyo sumu watachukuliwa hatua za kisheria”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
“Hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria, watakaotuhumiwa wote na wale ambao wamelima kwenye vyanzo vya maji pale kijijini na kuweka hiyo sumu watachukuliwa hatua za kisheria”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
No comments:
Post a Comment