Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
HALMASHAURI ya
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepokea zaidi ya shilingi bilioni 7.54 kwa
ajili ya kutekeleza programu ya uboreshaji wa Miji na Manispaa (ULGSP).
Ofisa habari wa
Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa fedha hizo ambazo zimepokelewa na
Manispaa hiyo zimetoka hazina kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kwamba zimeletwa
kwa awamu mbili.
Midelo alisema
kuwa fedha zilizoletwa kwa awamu ya kwanza zilipokelewa mwezi Mei mwaka huu, kiasi
cha shilingi bilioni 2.72 na awamu ya pili zilipokelewa Oktoba 6 mwaka huu kiasi
cha shilingi bilioni 4.82.
Alibainisha kuwa katika
mwaka wa fedha wa 2015/2016 Manispaa ya Songea kupitia programu ya ULGSP
ilipanga kutekeleza miradi yake minne ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara kiwango
cha lami kilometa 4.7 na fedha zingine zitatumika kwa ajili ya kuijengea uwezo halmashauri
hiyo.
Manispaa ya Songea
ni miongoni mwa halmashauri 18 hapa nchini, ambazo zinatekeleza mradi wa
uboreshaji wa Miji na Manispaa ambapo mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha
miaka mitano, kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018.
“Katika kipindi
cha miaka mitano halmashauri yetu Manispaa ya Songea imepanga kutekeleza miradi
nane yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 21’’, alisema Midelo.
Amelitaja lengo la
mradi huo kuwa ni kuziwezesha halmashauri zilizomo kwenye mradi, kuboresha
utendaji kazi kwa lengo la kutoa huduma bora na endelevu kwa jamii
inayohudumiwa.
Hata hivyo alisema
kuwa mradi umedhamiria kuongeza mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa mapato, kuimarisha
uzingatiaji wa sheria, kanuni na miongozo ya serikali, ujenzi wa miundombinu,
kuongeza uwajibikaji, usimamizi wa rasilimali za halmashauri na kujenga uwezo ndani
ya halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment