Vijana wakifanya kazi katika kiwanda cha kuzalisha tofari zilizochanganywa kwa simenti na mchanga ambacho kinaendeshwa na Kampuni ya Ovans Construction Limited, Mbinga mjini mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HATIMAYE Kampuni ya Ovans Construction Limited iliyopo Mbinga
mjini mkoani Ruvuma, imeanza kuzalisha tofari za kuchanganya mchanga na simenti
kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za aina mbalimbali, ikiwa ni lengo la kuwataka
vijana wanaojishughulisha na kazi ya ufyatuaji tofari za udongo mabondeni katika
mji huo waachane na kazi hiyo ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa
mazingira.
Aidha uhamasishaji huo wa vijana kuachana na kazi ya
ufyatuaji wa tofari za udongo mabondeni ni njia ya kuepukana pia na uharibifu
wa vyanzo vya maji ambao unaendelea kushika kasi kila siku katika mji huo.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Valence Urio alisema hayo juzi
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa ambapo alifafanua kuwa
kazi hiyo ya uundaji wa tofari za udongo pia huchangia kwa kiasi kikubwa
uharibifu wa misitu, ambapo wafyatuaji hulazimika kukata miti msituni kwa ajili
ya kuweza kupata kuni za kuchomea tofari.
Valence alisema kuwa baada ya kuona uharibifu huo wa
mazingira ukiwa unaendelea kushika kasi katika mji huo aliona ni vyema anunue
mashine ya kisasa ambayo itaweza kufanya kazi ya kufyatua tofari za kuchanganya
mchanga na simenti na kuwataka vijana wanaojishughulisha na kazi hiyo,
wajikusanye kwa pamoja na yeye atawasaidia kuunda kikundi ambacho kitasajiliwa
kisheria na kuweza kufanya kazi hiyo ya kuwaletea kipato.
“Ninahamasisha vijana wote hapa Mbinga waje kufanya kazi hii,
lengo waachane na kazi ya ufyatuaji tofari za udongo kule mabondeni kwani
huchangia kuharibu mazingira yetu”, alisema Valence.
Alisema mashine hiyo ambayo ujenzi wake umekamilika na sasa
kwa siku inauwezo wa kufyatua tofari za simenti (blocks) 1,600 hivyo anawaomba
Wadau na wananchi kwa ujumla kutoka ndani na nje ya Mbinga, kujitokeza kwa
wingi kununua tofari hizo ili waweze kukamilishia shughuli zao za ujenzi.
“Tofari tunafyatua kwa wingi kulingana na mahitaji ya mteja,
tunafyatua ukubwa wa inchi tano kwa tofari moja shilingi 1,100 na inchi sita
kwa shilingi 1,300 na kwamba mteja ambaye anaishi umbali usiozidi kilometa tano
kutoka eneo la kiwandani tunapofyatua tofari, tunamsafirishia bure sisi wenyewe
mpaka saiti katika eneo lake la ujenzi”, alisema.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo wa Kampuni ya Ovans Construction
Limited aliongeza kuwa, pia kampuni imeweza kusaidia vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga kuanzisha mradi wa ushonaji nguo na kusimamia
mikopo benki ya kikundi cha vijana kinachofahamika kwa jina la ‘Kusile
waendesha boda boda’ kilichopo mjini hapa, ili waweze kujipatia kipato na
kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika maisha yao.
No comments:
Post a Comment