Na Muhidin Amri,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amewataka viongozi wa vijiji na kata wilayani humo kuongeza uwajibikaji kwa
wananchi, hatua ambayo itasaidia kupata ushiriki mkubwa wa wananchi katika
shughuli za maendeleo.
Cosmas Nshenye, Mkuu wa wilaya ya Mbinga. |
Nshenye alisema hayo juzi Ofisini kwake, alipokuwa
akizungumza na mwandishi wa gazeti hili na kubainisha kuwa kuna haja sasa
kwa watendaji hao wa serikali kuona umuhimu wa kujituma ipasavyo, katika
kuwatumikia wananchi ambao bado wanakabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha
katika maeneo yao.
Pia Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, amewataka watumishi wote
wa umma kutokuwa chanzo cha matatizo na vurugu kwa wananchi kwani huu ni muda
wa kufanya shughuli za maendeleo na kujiepusha vitendo
viovu kama vile ulaji wa fedha za maendeleo zinazopelekwa katika
vijiji, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma za
kijamii.
Kadhalika Nshenye aliwataka kuwa wa wazi katika shughuli zao
za kila siku za kiutendaji ikiwa ni pamoja na kusoma taarifa za mapato na
matumizi, ambayo yamekuwa chanzo cha migogoro kwa baadhi ya watendaji ili waweze
kujijengea uaminifu na kukubalika kwa wananchi wanao waongoza.
Alisema kuwa, kumekuwa na malalkamiko mengi ya wananchi dhidi
ya viongozi wao pale ambapo wanashindwa kusoma taarifa hizo jambo ambalo
linasababisha kuzusha migogoro isiyokuwa na tija, ukizingatia kwamba kipindi
hiki cha serikali ya awamu ya tano kimedhamiria kuboresha huduma zake za
kijamii ili kuharakisha upatikanaji wa maendeleo hapa nchini.
“Kazi ya mtumishi wa umma ni kuwawezesha wananchi kuwa na mazingira
mazuri ambayo yatawafanya kupenda kushiriki katika kazi za kujitolea nguvu zao
kwa ajili ya maendeleo, kama vile zoezi linaloendelea nchini kote la
ufyatuaji tofari kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, nyumba
za walimu pamoja na zahanati na vituo vya afya kwa kila kijiji na kata”,
alisema Nshenye.
No comments:
Post a Comment