Na Muhidin Amri,
Songea.
WAUMINI wa Kanisa la AGAPE hapa mkoani Ruvuma, wametakiwa
kutoyumbishwa na Waumini wa madhehebu mengine kwa lengo la kuhama Kanisa hilo,
kwani imeelezwa kuwa endapo watafanya hivyo ni sawa na kuisaliti imani yao.
Askofu wa Kanisa hilo mkoani hapa, Asangalwisye Mwangakala alisema
hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa mara baada ya ibada
ya kuwasimika Wachungaji 17 watakaofanya kazi ya kueneza injili katika maeneo
mbalimbali mkoani humo.
Mwangakala alisema kuwa, hivi sasa kumekuwa na tabia kwa baadhi
ya waumini wa madhehebu mengine kuwarubini waumini wake ili waweze kulihama Kanisa
hilo, jambo ambalo likiendelea kufanyika linaweza kuleta chuki miongoni mwa Wakristo
mkoani hapa.
“Ninawaomba waumini wangu wasikubali kutanga tanga kutokana
na tamaa ya ushawishi fulani, bali yatupasa tuwe imara katika imani ya kanisa letu
na tusikubali kuyumbishwa na madhehebu mengine”, alisema.
Kwa mujibu wa Askofu huyo aliongeza kuwa baadhi ya waumini wa
madhehebu mengine wamekuwa na tabia ya kushawishi waumini wa kanisa lake
wajiondoe na kwenda kwao, kwa lengo la kutaka kuwavuruga hivyo wanatakiwa kuendelea
kuwa imara na kudumu katika imani yao.
Aliwataka waumini hao pamoja na wachungaji wapya, wakati wote
kuhakikisha kwamba wanadumisha umoja, amani na upendo miongoni mwao na
kujitokeza kushiriki kazi mbalimbali za kijamii katika misiba na hata kushiriki
katika ujenzi wa shughuli za kimaendeleo.
Pia amewataka kushiriki na kuhamasisha jamii juu ya suala la
kupeleka watoto wao shule, ili waweze kupata elimu na kumuunga mkono Rais Dkt.
John Magufuli katika vita dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe kazini na kuwafichua
watumishi wa umma wanaoendelea kufanya kazi kwa mazoea ili waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria kwa manufaa ya umma.
No comments:
Post a Comment