Sunday, October 23, 2016

ASKOFU NDIMBO AWATAKA WASOMI KUACHA KUBEZA JUHUDI ZINAZOFANYWA NA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

Wanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Augustivo wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wakiwa katika maandamano kuelekea ukumbini shuleni hapo jana wakati wa mahafali yao ya tano ya kidato cha nne.
Wanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Agustivo iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiimba wimbo wa shule yao wakati wa mahafali ya tano ya kidato cha nne katika shule hiyo.


Na Muhidin Amri,       
Mbinga.

WASOMI hapa nchini wametakiwa kutumia elimu yao katika kutafuta majawabu sahihi yatakayoiondoa Tanzania na tatizo la umaskini, kama anavyofanya Rais Dkt. John Magufuli badala ya kuwa mstari wa mbele kubeza na kukosoa juhudi hizo kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano.

Aidha imeelezwa kwamba, tabia hiyo ni fedheha kwao na haina tija kwa Watanzania wenzao kwani elimu waliyoipata, wametumia fedha za walipa kodi wa nchi hii kupata mikopo iliyowafanya waweze kutumiza malengo na ndoto zao.

Vilevile wamekumbushwa kutimiza wajibu wao na kujiepusha na tabia ya kuwakatisha tamaa baadhi ya wasomi wengine, ambao wapo tayari kutumia elimu na maarifa waliyonayo kwa faida ya Watanzania wenzao ambao bado wanakabiliwa na matatizo mengi, ikiwemo upungufu wa huduma muhimu za kijamii katika maeneo mbalimbali.


Hayo yalisemwa jana mjini Mbinga na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga John Ndimbo, katika hotuba yake iliyosomwa na Padri Joseph Mwingira wakati wa sherehe za mahafali ya tano ya Kidato cha nne shule ya Sekondari Augustivo iliyopo mjini hapa.

Padri Mwingira alisema kuwa katika suala la maendeleo ni lazima Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama, elimu na dini kuungana pamoja kuisaidia serikali  katika kumaliza matatizo yaliyopo ambayo yamekuwa  kikwazo kikubwa katika juhudi za kukuza uchumi, hivyo wakati umefika kwa wasomi  wa Tanzania kuacha kasumba ya kuikosoa serikali mara kwa mara hata pale inapofanya mambo  mazuri ya kimaendeleo.

Amewahimiza pia wazazi na walezi wa Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kupeleka watoto wao katika shule hiyo kwa kuwa ni yao na imekuwa na mchango mkubwa katika kuharakisha shughuli za maendeleo, kwani imekuwa ikitoa vijana wengi wasomi ambao wanatumikia wilaya hiyo katika sekta mbalimbali za kijamii.

“Hii shule ni yetu sisi wanambinga, ni muhimu kwa walezi na wazazi na hata jamii ya wanaruvuma kuchangamkia nafasi za masomo kwa ajili ya kuleta watoto wetu hapa waweze kupata elimu bora, ambayo itasaidia kupata vijana wengi wasomi”, alisema.

Pia amewakumbusha watoto wanaomaliza kidato hicho cha nne, kutumia muda mchache uliobaki kabla ya kufanya mitihani yao ya mwisho kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri, hatua ambayo itawasaidia kuweza kutimiza ndoto walizonazo za kuendelea na elimu ya kidato cha tano na hata kufika chuo kikuu.

Alisema kuwa kutokana na thamani ya elimu hivi sasa kamwe wasiridhike na elimu ya kidato cha nne, bali wanapaswa kuwa na dhamira ya kufika mbali hatua itakayowasaidia kuwa na uhakika wa kupata ajira na kuweza kukabiliana na changamoto za maisha yao ya baadaye.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari Augustivo Mussa Mdaka mbali na kuwapongeza wahitimu hao wa kidato cha nne alisema kuwa, kitaaluma shule yake ina mafanikio makubwa ya ndani  na nje ya shule kiwilaya, mkoa na hata taifa.

Alisema kuwa matokeo ya mitihani mbalimbali yameendelea kuwatia hamasa na kuonesha tumaini bora kwa wanafunzi na wazazi, jambo ambalo limeifanya shule hiyo kuwa kisiwa cha elimu kwa kushika nafasi ya 10 bora kiwilaya na kimkoa kushika nafasi ya tisa kati ya shule 100, kitaifa nafasi ya 283 kati ya 3,452. 

Alisema kuwa kwa upande wa ufundishaji wa somo la kompyuta, wanategemea kuanza kufundisha siku chache zijazo kwani hadi sasa shule tayari imeshanunua kompyuta 20 na imepata nyingine 20 kutoka shirika la Mission of Afrika Tanzania (MIATA) na kufikia jumla yake kuwa 40.

Mussa alisema kuwa changamoto iliyopo sasa ni kompyuta mpakato za walimu (Laptop) na Projector ambavyo kama vingekuwepo vingerahisisha sana mchakato wa kutoa elimu na maarifa toka kwa walimu kwenda kwa wanafunzi.

Naye mkurugenzi wa shule hiyo Joseph Mdaka, ameahidi kutoa shilingi milioni 2 kwa wanafunzi 10 watakaopata alama A katika matokeo yao ya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.

Akitangaza zawadi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi huyo, mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Exaud Mahenge alisema kuwa ahadi hiyo ya fedha anataka iwe kama chachu kwa wahitimu hao kutumia muda wao uliobaki, kujisomea kwa bidii, juhudi na maarifa na hatimaye kufanya vyema katika mitihani yao ya kitaifa.

Shule ya Sekondari Augustivo ni shule ya kwanza yenye kidato cha kwanza hadi cha sita kumilikiwa na mtu binafsi wilayani humo ambaye ni mzawa wa wilaya ya Mbinga, ambapo imesaidia kwa kiasi kikubwa vijana wengi ndani na nje ya wilaya hiyo kwa wanaokosa nafasi ya kujiunga na shule za sekondari za serikali  kupata elimu hiyo.

No comments: