Na Kassian
Nyandindi,
Iringa.
WAANDISHI wa habari hapa nchini, wametakiwa kujijengea
ujasiri na kuacha kukata tamaa pale wanapokumbwa na vikwazo wakati wanapofanya
kazi zao, badala yake wazingatie maadili ya taaluma yao ili jamii iendelee kuwathamini
na kuheshimu vyombo vya habari.
Aidha imeelezwa kuwa tasnia ya habari, ndiyo fani mtambuka
inayoweza kuwafanya wananchi waweze kusonga mbele kimaendeleo kwa faida ya
kizazi cha sasa na hapo baadaye.
Mwenyekiti wa taifa, Shirika la Karibu Tanzania Association
(KTA) Aidan Mchawa alisema hayo leo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tatu ya
Wanahabari na Wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) hapa nchini,
yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Neema Craft uliopo katika Manispaa ya Iringa mkoani
hapa.
“Kama tasnia hii ya habari isingelikuwepo hakika dunia
ingebakia kuwa madudu, Waandishi wa habari wanamchango mkubwa katika jamii na
ndio maana maeneo mengi, tunashuhudia matatizo yanayoibuliwa na hawa wenzetu na
serikali imekuwa ikichukua hatua za haraka kwa ajili ya manufaa ya taifa letu”,
alisema Mchawa.
Kadhalika alieleza kuwa KTA ni shirika lisilokuwa la serikali
ambalo ni mwamvuli wa Vyuo vya maendeleo ya wananchi Tanzania, limekuwa
likifanya kazi na vyuo hivyo kwa kushirikiana na serikali kwa lengo la
kusimamia na kuvifanya viweze kusonga mbele katika masomo na fani mbalimbali
zinazotolewa vyuoni humo.
Awali kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Shirika hilo,
Maggid Mjengwa alisema kuwa lengo la kuwakutanisha Waandishi wa habari katika
mafunzo hayo ni baada ya kuona ni watu ambao wakiungana na Wakufunzi wa vyuo
hivyo, wataweza kuijenga nchi na kuendeleza jamii katika tasnia ya habari.
“Ndugu zangu Waandishi wa habari baada ya mafunzo haya
mtakwenda pia kusaidia kutoa elimu katika hivi vyuo vyetu vya maendeleo ya
wananchi, malengo yetu ni kuifanya jamii itambue pia umuhimu wa tasnia hii ya
habari na mafunzo haya yana umuhimu mkubwa katika vyuo vyetu”, alisema Mjengwa.
No comments:
Post a Comment