Baadhi ya akinamama wajawazito wakiwa katika eneo la hospitali ya wilaya ya Mbinga. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepiga
hatua katika kupunguza vifo vya akima mama wajawazito na watoto chini ya
umri wa miaka mitano kutoka vifo 140 kati ya 100,000 kwa mwaka 2013 hadi
kufikia vifo 40 mwaka 2015 hatua ambayo imeleta matumaini makubwa, kwa
akina mama hao na jamii kwa ujumla wilayani humo.
Mafaniko hayo yametokana na mkakati kabambe wa
halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo ndani na nje ya
wilaya hiyo ambao wamejiwekea, katika kuimarisha mfumo wa rufaa kwa akina mama
wajawazito na kuwapatia elimu ya matunzo kwa wajawazito hao kuhusu umuhimu wa
kuhudhuria Kliniki mapema na wakati wote wa ujauzito wao na mara baada ya
kujifungua.
Pia elimu ya kujifungulia katika vituo vya afya na hospitali
nao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo kwa akina mama hao pamoja na
watoto wao, kwani pale wanapohitaji kutoka katika ngazi ya zahanati au
kituo cha afya huchukuliwa kwa gari maalumu la kubebea wagonjwa bila malipo
yoyote, tofauti na siku za nyuma walikuwa wakilazimika kuchangia kidogo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo
Samandito alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya
mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo ya afya na changamoto zinazoikabili
hasa baada ya serikali kuigawa halmashauri hiyo na kuzaliwa kwa halmashauri
nyingine ya mji wa Mbinga.
Samandito alifafanua kuwa kupungua kwa idadi ya vifo vya
akina mama wajawazito ni faraja kubwa sio kwa wanawake wenyewe tu, bali hata
kwa serikali ambayo imekuwa ikiboresha huduma mbalimbali za afya kwa wananchi
wake kwa lengo la kuwa na kizazi chenye afya kitakachoweza kushiriki kikamilifu
katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Alisema kuwa mafanikio hayo yanatokana na mikakati
iliyojiwekea halmashauri hiyo kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, ugawaji
wa vyandarua, huduma ya dawa za ARV’s kwa akina mama wajawazito ambao
wanamaambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi, kuongezeka kwa vituo vya afya sambamba na
kuboresha upatikanaji wa huduma ya damu salama katika vituo maalumu
vilivyopendekezwa kutoa huduma hiyo.
Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa juhudi na nguvu ya
pamoja kati ya halmashauri na wananchi ambao kwa namna moja au nyingine,
wamekuwa mstari wa mbele katika kujitolea na kuchangia shughuli mbalimbali
katika maendeleo licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi za maisha yao ya kila
siku.
Aidha aliongeza kuwa katika suala la kupungua kwa vifo vya
akina mama wajawazito, lakini pia halmashauri hiyo imefanikiwa kupunguza vifo
vinavyotokana na ugonjwa hatari wa malaria ambao umekuwa ukiua watu wengi hapa
nchini, kwani wilaya ya Mbinga imepunguza kutoka vifo 471 mwaka 2012 hadi
kufikia vifo 42 mwaka 2014 na kwamba hivi sasa hadi kufikia mwezi Disemba
mwaka 2015 idadi hiyo ilizidi kupungua hadi kufikia vifo 20 na hayo yametokana
na dhamira ya dhati ya wilaya hiyo iliyojiwekea katika kupambana na magonjwa
hayo.
Hata hivyo hata ugawaji wa vyandarua vyenye dawa umesaidia
pia kupunguza ugonjwa huo katika wilaya ya Mbinga ambao ulikuwa ukiambatana na
utoaji wa hati punguzo zaidi ya 20,015 ambazo zilizotolewa kwa akina mama
wajawazito ambapo ni sawa na asilimia 89.5 huku vyandarua vilivyotolewa
vimefikiaidadi ya 150,058 kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano na kwamba
mwaka 2015 tayari ilishagawa vyandarua zaidi ya 250,169 kwa watoto wenye umri
wa miaka mitano na kuendelea.
No comments:
Post a Comment