Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imeanza
kutekeleza mpango wake wa zoezi la upimaji ardhi katika maeneo ambayo yana
rasilimali muhimu za kudumu kama vile mashamba ya kahawa na miti, ili kuweza
kuyaongezea thamani na kuwafanya wakulima waweze kupata mikopo katika taasisi
za kifedha na hatimaye waweze kuondokana na umaskini.
Aidha imeelezwa kuwa mpango huo unalenga kupima ekari zaidi
ya 68,000 na kwamba mpaka sasa tangu zoezi hilo lianze tayari ekari 12,600
zimepimwa na kwamba kazi hiyo imefanyika katika kipindi cha wiki moja.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya
hiyo, Gombo Samandito alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ambao
walitembelea katika baadhi ya vijiji, ambavyo zoezi hilo la upimaji linaendelea
kufanyika.
Samandito alisema kuwa zoezi hilo linaenda sambamba na upimaji
wa miji midogo ambapo katika wilaya ya Mbinga tayari miji yake mitano ya
Kigonsera, Ruanda, Matiri, Mkako na Kiamili kazi inaendelea ya uchukuaji wa
takwimu za awali katika maeneo yenye nyumba na viwanja.
“Kazi za kiutendaji zaidi wa kiofisi ikiwemo uaandaji wa
ramani za msingi (Base map) unaendelea kufanyika, tuna makampuni matano ambayo
yanafanya kazi hii ya upimaji”, alisema Samandito.
Alifafanua kuwa hapo baadaye baada ya kukamilisha zoezi la
upimaji mashamba yenye mazao hayo ya kudumu kama vile kahawa na miti, pia
watapima kwenye mashamba ambayo yana mazao ya muda ikiwemo mahindi na
mengineyo.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa mpaka sasa kati ya
kata 29 zilizopo wilayani humo tayari kata 20 zimeanishwa kwa ajili ya zoezi
hilo la upimaji wa ardhi ya wananchi wake ili waweze kupata hati miliki za
kimila ambazo ni kata ya Kipapa, Langiro, Maguu, Mapera, Kambarage, Mikalanga,
Nyoni, Mpapa, Mbuji, Litembo, Kitura, Ngima, Wukiro, Kipololo, Ukata, Linda,
Mkumbi, Kihangimahuka, Lukarasi na Matiri.
No comments:
Post a Comment