Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WENYEVITI na Watendaji wa vijiji na kata katika Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamenyoshewa kidole na kuelezwa kuwa katika
maeneo yao ya kazi wamekuwa hawasomi taarifa za mapato na matumizi na kuwafanya
wananchi walalamikie hali hiyo, huku baadhi ya maeneo wengine wakigomea hata
kushiriki katika kufanya shughuli za maendeleo.
Aidha imefafanuliwa kuwa kutokana na tatizo hilo kuendelea
kushamiri na kuwa kero katika jamii, kuna kila sababu sasa kwa uongozi wa
halmashauri hiyo kupitia kitengo chake cha ukaguzi wa ndani kumpeleka mkaguzi
huyo ili aweze kufanya ukaguzi katika vijiji na kata zote, ambazo kuna taarifa
zenye utata juu ya mapato na matumizi ya fedha za wananchi.
Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo walilalamikia hali
hiyo juzi kwa nyakati tofauti, katika kikao chao cha baraza la madiwani
kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya
hiyo, Vivian Mndolwa alisema kuwa tayari hatua za ukaguzi zimeanza kuchukuliwa
katika baadhi ya vijiji na kata ambazo zimeonesha kuwa na matatizo hayo, huku
akisema kazi hiyo imekwisha fanyika katika vijiji vya Ntunduaro, Myao na kata
ya Ruanda.
Mndolwa aliongeza kuwa kutokana na uwepo wa uhaba wa
rasilimali fedha na watumishi katika idara ya ukaguzi, wamekuwa wakiendelea na
ukaguzi kwa awamu na taarifa zitaendelea kutolewa kwa kila kaguzi inapofanyika
kupitia vikao husika.
“Pale Diwani anapogundua kwamba kuna tatizo ni vizuri atoe
taarifa mapema katika ofisi ya Mkurugenzi, ili ofisi yetu ya ukaguzi iweze kuchukua
hatua haraka na kumaliza migogoro iliyopo huko’, alisisitiza Mndolwa.
No comments:
Post a Comment