Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akisisitiza jambo katika kikao chake alichokifanya hivi karibuni wilayani Mbinga mkoani humo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AGIZO limetolewa kwa viongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma wahakikishe kwamba, wanasimamia kikamilifu na kumaliza haraka
iwezekanavyo mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa
kijiji cha Mihango kata ya Kigonsera wilayani humo na mwekezaji tarajiwa wa Kampuni
ya AVIV Tanzania Limited.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge alitoa agizo
hilo juzi alipokuwa katika kikao chake cha kazi na viongozi wa wilaya hiyo,
kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga iliyopo mjini hapa.
“Suala hili la mwekezaji natoa wiki mbili liwe limekamilika
na taarifa kamilifu niipate haraka ofisini kwangu, nataka zingatieni kama
taratibu za kutwaa eneo hili za wananchi zilifuatwa au la”, alisema Dkt.
Mahenge.
Kadhalika Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa hataki kuona
jambo hilo linalazimishwa au kukumbatiwa na viongozi wa serikali kwa kumbeba
mwekezaji huku wananchi wakilalamika, badala yake amewataka wachukue maamuzi
yenye busara ili kuweza kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza hapo
baadaye.
Alisema kuwa anataka kuona mwananchi anatoa ardhi yake kwa
kuridhika mwenyewe na sio kulazimishwa na kwamba wakati wa kutekeleza suala
hilo ameagiza haki itendeke na ofisi yake, ipelekwe taarifa kamili juu ya idadi
ya watu wangapi wanaokubali kutwaa ardhi yao na wale wasiokubali kupitia vikao
husika vitakavyowashirikisha wananchi hao.
Mnamo mwaka 2014/2015 Kampuni ya AVIV Tanzania Limited
ilitafuta eneo katika kijiji cha Mihango kata ya Kigonsera wilayani Mbinga, kwa
lengo la kutaka kuzalisha zao la kahawa ambapo wananchi wengi wa kijiji hicho
mpaka sasa hawataki kutoa ardhi yao kwa mwekezaji huyo kwa kile wanachoeleza
kuwa watakosa eneo la kuzalisha mazao yao ya chakula na biashara na sehemu za
kuishi, kutokana na wengi wao kuwa wahamiaji kutoka maeneo mengine ndani ya
wilaya hiyo.
Wananchi wa kijiji hicho wanadai pia mwekezaji huyo hajafuata
taratibu za utwaaji wa ardhi yao, hivyo hali hiyo ilisababisha kuleta mgogoro mkubwa
uliodumu kwa muda mrefu kati ya uongozi wa wilaya, mwekezaji na wananchi hao
hatua ambayo ilipelekea hata viongozi wa kata hiyo hivi karibuni kufanyiwa
vurugu kwa kupigwa mawe na wananchi wa kijiji hicho wakati mwekezaji huyo
alipoonekana akipita katika maeneo yao.
No comments:
Post a Comment