Friday, October 21, 2016

KATIBU TAWALA MBINGA ASISITIZA UUNDAJI WA MABARAZA YA WATU WENYE ULEMAVU


Baadhi ya Watu wenye ulemavu wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Gilbert Simiya ambaye amevaa shati la kitenge, mara baada ya kufanya uzinduzi wa mradi wa mafunzo ya sheria ya watu wenye ulemavu. (Picha na Muhidin Amri)
Na Kassian Nyandindi,          
Mbinga.

MAOFISA maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya wilaya na mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhakikisha kwamba wanasimamia ipasavyo zoezi la uundwaji wa mabaraza ya watu wenye ulemavu katika ngazi ya halmashauri, kata na vijiji.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga, Gilbert Simiya alipokuwa kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa mafunzo ya sheria namba 9 ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010, uliofanyika kwenye ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini hapa.

“Natoa agizo kwenu, uundwaji wa mabaraza haya ni suala la lazima tekelezeni hili mapema na kwa wakati uliopangwa, ili serikali iweze kufikia malengo yake katika makundi yote ya watu wenye ulemavu”, alisisitiza.

Simiya aliongeza kuwa utekelezaji wa zoezi hilo ni agizo lililotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hivyo muda wowote serikali itakuja kufanya ufuatiliaji juu ya utekelezaji wake.

Alisisitiza kuwa  utekelezaji wa jambo hilo lisiwe kwa mtindo wa kupika anataka kuona linafuata misingi na taratibu zilizowekwa, ili kuweza kuwatendea haki walemavu wa wilaya hiyo na kwamba malengo ya uundwaji wa mabaraza hayo ni kutaka kuwatambua walemavu na shughuli zao wanazozifanya.


Vilevile akizungumzia juu ya mradi wa mafunzo hayo ya watu wenye ulemavu ambayo yamefadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civil Society, Katibu tawala huyo alisisitiza juu ya nidhamu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na shirika hilo kwa ajili ya kuendeshea mafunzo hayo, ili kuweza kuondoa migongano isiyokuwa ya lazima.

Awali kwa upande wake akitoa taarifa fupi ya mradi wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Chama Cha Walemavu (CHAWATA) wilayani hapa, Martin Mbawala alisema kuwa shirika hilo limeweza kutoa fedha shilingi milioni 21,000,000 kwa lengo la kutoa mafunzo ya sheria namba 9 ya mwaka 2010 kwa watu wenye ulemavu ili jamii iweze kutambua haki, wajibu na mahitaji yao kwa kundi hilo tete.


Mbawala alifafanua kuwa mafunzo hayo yataendeshwa katika kata ya Ruanda halmashauri ya wilaya Mbinga na Mpepai iliyopo kwa upande wa halmashauri ya mji wa Mbinga wilayani humo, katika kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Oktoba mwaka huu hadi Marchi 2017 ambapo baada ya mafunzo hayo kutakuwa na mikutano miwili ya hadhara kwa kila kata ikilenga uhamasishaji kwa jamii kuhusiana na sera, sheria na haki za watu wenye ulemavu.

No comments: