Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lijombo wilayani humo. |
Na Muhidin Amri,
Tunduru.
MKUU wa wilaya ya Tunduru Juma Homera, ametoa siku saba kwa
viongozi wa kijiji cha Lijombo wilayani humo kuhakikisha kwamba wanarejesha fedha
kiasi cha shilingi 999,500 ambazo waligawana, huku wakijua kwamba fedha hizo ni
za serikali ambazo zililenga kutekeleza miradi ya maendeleo
kijijini humo.
Homera alitoa agizo hilo juzi wakati alipokuwa akizungumza katika
mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho, ambao ulilenga kutatua mgogoro uliodumu
kwa muda mrefu kati ya wananchi na viongozi wao wa kijiji juu ya ubadhirifu wa
fedha za miradi ya maendeleo.
Kijiji cha Lijombo kimeingia katika mgogoro huo kufuatia
wananchi hao kuwatuhumu viongozi wao, kwa matumizi mabaya ya madaraka
ikiwemo kutafuna fedha pamoja na kushindwa kutoa taarifa za mapato na
matumizi na kusababisha wananchi kugoma kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru amewataka viongozi hao
kurudisha haraka fedha hizo kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria, kwani
wamesababisha kusimama kwa baadhi ya miradi kutokana na vitendo hivyo vya
ubadhirifu wa fedha za wananchi.
Pia Homera ameagiza kwamba kuna fedha shilingi 300,00 ambazo
walipewa kwa ajili ya kuwasaidia wazee nazo zirejeshwe haraka, kupitia akaunti
ya kijiji hicho ili walengwa waweze kupewa na ziwasaidie katika kujikwamua kwenye
maisha yao.
Awali wakitoa malalamiko yao kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu
huyo wa wilaya wananchi hao walisema kwamba mambo hayo yanayofanywa na viongozi
wao ndiyo chanzo kikubwa cha kuathiri maendeleo ya wananchi, yasiweze kusonga
mbele kutokana na kukosa uaminifu hasa katika matumizi ya fedha zinazotolewa na
serikali.
Walibainisha kuwa wamekuwa na mazoea viongozi wao kujifungia
ofisini peke yao na kutoa maamuzi bila kushirikisha wananchi, ndiyo maana
wanalalamikiwa na wananchi kufikia hatua hata ya kususia kufanya shughuli za
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment