Ofisi za Halmashauri Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
imelalamikiwa kwa kushindwa kwake kutenga maeneo rasmi ya maegesho ya magari
hususani Malori na pikipiki, kitendo ambacho hivi sasa kinasababisha msongamano
mkubwa wa vyombo hivyo vya moto kwa watu wanaotembea kwa miguu.
Pikipiki maarufu kama Yeboyebo, bajaji na magari ya mizigo
yamekuwa yakipaki hovyo bila kufuata utaratibu maalumu katika maeneo mbalimbali
ya Manispaa hiyo kama vile eneo maarufu la Ikweta, ambalo kuna makazi ya watu
na nyumba za ibada.
Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wakazi
hao walisema kuwa hali hiyo inawasababishia usumbufu mkubwa wakati wanapohitaji
huduma ya usafiri kwani hakuna maeneo rafiki ambayo Manispaa hiyo imetenga kwa
ajili ya kupata huduma ya usafiri kama vile boda boda, bajaji na malori.
Walisema kuwa kutokana na madereva hao kuachwa kiholela, kunawafanya
wakati mwingine kuwa na hofu kutokana na hasa kwa madereva wa pikipiki
kujihusisha na vitendo vya wizi, kwani wengi wao hawana sare na wamekuwa wakiendesha
shughuli zao kwa kutembea barabarani.
Mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Songea, Ally Ngonyani alieleza
kuwa tangu Manispaa hiyo iwahamishe madereva wa bajaji eneo la Soko kuu na wale
wa malori kutoka katika eneo la mtaa wa Majengo mitumbani kumekuwa na usumbufu mkubwa,
hatua ambayo inawafanya abiria washindwe kutumia usafiri huo ambao awali
ulikuwa ni rahisi zaidi kwao.
“Pia tuna hofu kubwa ya kugongwa na boda boda, kwa sababu
boda boda nyingi hazitulii katika eneo maalumu badala yake hutembea hovyo
mitaani kwa ajili ya kutafuta wateja, jambo ambalo limekuwa likisababisha ajali
nyingi na za mara kwa mara”, alisema Ngonyani.
No comments:
Post a Comment