Na Kassian Nyandindi,
Songea.
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Songea
mkoa wa Ruvuma, kimewavua madaraka wanachama wake sita na wajumbe watano wa Kamati tendaji ya chama hicho wilayani humo kwa muda wa miezi 30.
Imefafanuliwa kuwa kuvuliwa madaraka kwa wanachama na wajumbe
hao, kumetokana na kudaiwa kwamba walikihujumu chama hicho wakati wa uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana na kusababisha mgombea Ubunge kupitia tiketi
ya CHADEMA Jimbo la Songea mjini, Joseph Fuime kushindwa kupita katika chaguzi
hizo.
Freeman Mbowe, Mwenyekiti CHADEMA Taifa. |
Akizungumza waandishi wa habari mjini hapa, Katibu wa Chama
cha demokrasia na maendeleo mkoa wa Ruvuma, Delphin Gazia alisema kuwa
wanachama hao wamevuliwa uanachama tangu Septemba 14 mwaka huu kutokana na
sababu hizo.
Gazia aliwataja wanachama hao waliofutwa kwenye daftari la
orodha ya wanachama kuwa ni Rhoda Komba aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake
(BAWACHA) wilayani songea, ambaye pia katika kipindi kilichopita alikuwa ni
diwani wa viti maalum toka kata ya Mfaranyaki Manispaa ya Songea na Seiph Ahmed
Seiph ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la wazee la wilaya hiyo.
Wengine ni Omary Hassan ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza
la Vijana (BAVICHA) wilayani humo, Ajaba Nditti na Swedi Millanzi ambao
walikuwa ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya wilaya na Emmanuel Kalisinje
ambaye alikuwa mjumbe kamati ya utendaji ambapo alivuliwa uanachama huo,
akidaiwa kutenda kosa la kuiba nyaraka muhimu za chama na kuzipeleka kwa
makada wa vyama vingine vya siasa.
Alisema kuwa wanachama hao waliovuliwa uanachama kuanzia
ssa hawataruhusiwa kufanya shughuli ya aina yoyote ya chadema kwani
imebainika kuwa ndio waliokihujumu chama kwenye kipindi cha kampeni hadi
siku ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi.
Katibu huyo wa CHADEMA alieleza kuwa wakati wa kipindi cha kampeni
chaguzi zilizopita, kiliunda tume maalumu ambayo ilipewa jukumu la kuratibu
shughuli mbalimbali za uchaguzi mkuu, lakini timu hiyo cha kushangaza badala ya
kusimamia shughuli za chama iliamua kufanya tofauti na wakati wote ikitoa siri
za chama hicho kwa vyama vingine vya siasa jambo ambalo lilisababisha mgombea
ubunge kupitia chama hicho jimbo la Songea mjini kushindwa.
Gazia alisema kuwa inaonesha wazi kuwa kulikuwa na figisu
figisu walizozifanya ambazo zilitoa nafasi kwa mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kutangazwa kuwa ndiye aliyekuwa mshindi kwenye uchaguzi huo, kwani
mgombea ubunge wa CHADEMA baadaye ilibainika kuwa ndiye aliyepata kura
nyingi tofauti na tangazo lililotolewa na Mkurugenzi wa uchaguzi wa jimbo
la Songea mjini, Raphael Kimari.
Alifafanua kuwa mgombe ubunge kupitia CHADEMA Fuime alipata
kura 40,766 na jumla ya wapiga kura walikuwa 77,554 lakini wakati wa
kutangazwa matokeo takwimu hizo hazikutajwa na mgombea
alipotakiwa apeleke nakala za matokeo ya uchaguzi huo, alikataa jambo ambalo
linaonesha kuwa kulikuwa na mchezo mchafu uliofanyika.
Wengine waliosimamishwa uanachama kwa muda wa miezi 30 kwa
makosa ya utovu wa nidhamu wakituhumiwa kupita kila kata za chama hicho kuwashawishi
vijana kufunga ofisi za CHADEMA na kupanga njama za mapinduzi kwa viongozi
wa chama hicho ngazi ya wilaya Songea, kuwa ni Sikitu Sallum ambaye
alikuwa Katibu wa BAVICHA wa wilaya hiyo na Zuberi Tindwa ambaye alikuwa
ni mhamasishaji ndani ya chama hicho.
Katibu huyo wa Chama cha demokrasia na maendeleo mkoa wa
Ruvuma, Gazia alifafanua kuwa pamoja na viongozi hao kuwavua uanachama bado
kamati ya utendaji ya mkoa inaendelea kufuatilia mwenendo wa Kampeni za
uchaguzi Mkuu uliopita ili kuweza kuchukua hatua zaidi kwa aliyekuwa mgombea wa
ubunge jimbo la Songea mjini kupitia tiketi ya chama hicho, Fuime ambaye
alisimamishwa miezi kadhaa iliyopita baada ya kukaidi kuleta nakala halisi za
matokeo ya uchaguzi huo mwaka jana.
No comments:
Post a Comment