Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepanga
kutekeleza miradi nane iliyopo chini ya mradi wa uendelezaji miji na manispaa,
katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 kwa lengo la kuwaletea
maendeleo wananchi wake kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Hii ni moja kati ya sehemu ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. |
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Manispaa
hiyo, Albano Midelo alisema kuwa Manispaa hiyo ni miongoni mwa halmashauri 18
hapa nchini ambazo zinatekeleza mradi huo ambao unasimamiwa na serikali ya
Tanzania kwa ushirikiano na benki ya dunia.
Midelo alisema kuwa Manispaa ya Songea, inatarajia kutumia
zaidi ya shilingi bilioni 21.8 katika kutekeleza miradi ya uendelezaji miji yake
na manispaa hiyo ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu.
Vilevile Raphael Kimary ambaye ni mchumi Mkuu wa Manispaa ya
Songea, aliitaja miradi hiyo kuwa ni ya ukarabati wa barabara kwa kiwango cha
lami kilometa 15 ambayo itagharimu shilingi milioni 11.5 na ununuzi wa magari
ya kuzolea taka, yatakayogharimu shilingi bilioni 1.14.
Miradi mingine ni ujenzi wa stendi mpya ya magari ya abiria
(mabasi) katika eneo la shule ya Tanga mjini hapa, kwa gharama ya shilingi
bilioni 5 na ujenzi wa machinjio ya kisasa itakayogharimu shilingi bilioni 2.1.
Vilevile katika utekelezaji huo kutakuwa na ukarabati wa
dampo la kuchomea taka kwa gharama ya shilingi bilioni1.5, kujenga uwezo
watumishi na viongozi wa kisiasa kwa gharama ya shilingi milioni 200 na
ukarabati wa bustani ya manispaa hiyo kwa shilingi milioni 300.
Kimary amezitaja changamoto zinazosababisha miradi kushindwa
kutekelezwa kwa wakati ni kutokana na kutopatikana kwa fedha za miradi kwa muda
uliopangwa, kuchelewa kupata kibali cha athari za mazingira katika maeneo
ambayo miradi inatekelezwa toka Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC) jambo
ambalo linasababisha kuchelewa kuanza kazi husika.
Baraza la madiwani wa halmashauri ya Manispaa ya Songea
wameunga mkono juu ya taarifa ya utekelezaji wa program hiyo ya uendelezaji wa
manispaa hiyo na kushauri pia mradi wa bustani ya manispaa hiyo, ufanyiwe ukarabati
mapema kwani nao imekuwa ni chanzo cha mapato kutokana na wakazi wengi wa
Songea kununua miche ya miti inayozalishwa hapo na kwenda kuipanda katika
maeneo yao kwa lengo la kutunza mazingira.
No comments:
Post a Comment