Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MVUTANO uliodumu kwa muda mrefu baina ya Wadau wa
usafirishaji abiria pamoja na baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali ya mkoa
wa Ruvuma, ambao ulihusisha matumizi ya vituo viwili vikubwa vya mabasi ya
abiria mjini Songea umeelezwa kumalizika, baada ya kufanyika mazungumzo na kuwepo
kwa makubaliabo ya pamoja kwa pande zote husika.
Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika Kituo cha
mabasi mjini hapa, ambao ulishirikisha baadhi
ya Wadau hao, abiria na wananchi, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea
Abdul Mshaweji pamoja na Mbunge wa jimbo la Songea mjini, Leonidas Gama alisema
kwamba baada ya mazungumzo yaliyochukua muda mrefu na kuibuka kwa msuguano juu
ya matumizi ya vituo vikubwa viwili, yamemalizika kwa makubaliano yaliyoridhiwa
na viongozi watano wa ngazi za juu katika mkoa na halmashauri hiyo ya Manispaa.
Mshaweji alisema kuwa vikao hivyo vilimhusisha Mkuu wa mkoa
wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge, Katibu tawala wa mkoa huo Hassan Bendeyeko, Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea Tina Sekambo, Mstahiki Meya wa Manispaa
hiyo, Abdul Mshaweji na Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas Gama ambapo pamoja
wamekubaliana kuwa vituo vyote viwili vya mabasi ya abiria vitumike ambavyo ni kile
kituo kilichopo mjini kati na cha Msamala.
Alifafanua kuwa uamuzi huo ambao ndiyo unasimamiwa na
halmashauri hiyo ya Manispaa, uliamuriwa kwenye vikao halali vya baraza la
madiwani wakati walipopata mkopo kutoka benki ya dunia kwa ajili ya kufanyika
ukarabati wa kituo kikuu cha mabasi cha mjini kati, na kuanzishwa kwa kituo cha
muda cha Msamala ili kupisha ukarabati huo uweze kufanyika.
Pia aliwaomba radhi wananchi kwa kuwepo kwa mvutano huo
uliowaweka njia panda kwa muda mrefu kati ya wananchi wa Manispaa hiyo na nje
ya manispaa, kushindwa kuelewa hatima ya uwekezaji wao walioufanya kwenye vituo
vyote viwili.
Kwa ujumla mazungumzo hayo na makubaliano ya pamoja
yalipofanyika na kuafikiana kuwa vituo vyote viwili vya mabasi vitumike kwa
mabasi yanayotoka nje ya mkoa kuanzia safari zake, kwenye kituo cha mjini kati na
kupitia kituo cha Msamala na kuendelea na safari huku yale yanayoingia kuanzia
kituo cha Msamala na kumalizia safari zake kwenye kituo cha hapa mjini.
Naye Mbunge wa jimbo hilo Leonidas Gama alisema kuwa maamuzi
hayo yana baraka zote kwa sababu yamefanyika kwa kuzingatia maslahi mapana ya
wananchi wa mkoa wa Ruvuma, pamoja na wageni wanaoingia na kutoka kwenye mkoa
huo hivyo hakuna mshindi katika maamuzi hayo bali maslahi ya makundi yote ya
wananchi ndiyo yaliyozingatiwa zaidi.
Hata hivyo pamoja na viongozi hao kutoa tamko hilo la
kuruhusu kituo hicho cha mjini ambacho siku za karibuni kilianza kutumika kwa
ajili ya daladala, kianze kutumiwa na mabasi makubwa ya abiria yanayoenda nje
ya mkoa jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, limeendelea kuyazuia mabasi hayo kuingia
kwenye kituo hicho kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria kwa kile
kilichoelezwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Zubery Mwombeji kwamba Jeshi hilo
linasimamia maamuzi yalitotolewa awali na halina taarifa ya mabadiliko hayo.
No comments:
Post a Comment