Msimamizi wa
ujenzi wa kiwanda cha kusindika nafaka cha Leop and Viann Associates Tanzania
Limited, Zeno Komba akitoa maelekezo namna ambavyo mtambo wa kusindika mahindi unavyofanya
kazi.
|
Hapa Zeno
Komba akitoa maelekezo juu ya namna ambavyo kipimo cha kielektroniki
kinavyofanya kazi wakati wa upimaji mahindi kiwandani hapo.
|
Na Dustan Ndunguru,
SERIKALI inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imekuwa ikiendelea
na jitihada zake za kuhamasisha Watanzania wazalendo, kujenga dhana ya kuwekeza
katika ujenzi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa hapa nchini hali ambayo
itaifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Ukiachilia mbali Wazalendo, pia inaendelea kuhamasisha wawekezaji
kutoka nje ya nchi waweze kuja kuwekeza kwa kujenga viwanda hivyo ambapo katika
kufanikisha hilo, serikali inaowajibu wa kuandaa mazingira mazuri ambayo
hayatakuwa kikwazo katika kufanikisha zoezi hilo muhimu la uwekezaji.
Watanzania waliowengi wanayo mitaji midogo ambayo kimsingi
wanaweza kujikita zaidi katika uanzishaji wa viwanda vidogo nchini kote,
ikiwemo maeneo ya vijijini ambako wakulima wamekuwa wakizalisha mazao
mbalimbali huku yakishindwa kupata bei nzuri kutokana na kukosa uwezo wa
kuyasindika na hivyo kuyaongezea thamani.
Viwanda vidogo ndiyo vyenye uwezo wa kutoa ajira kwa watu wa
kada ya chini kwa wingi, ikilinganishwa na viwanda vikubwa ambavyo sehemu kubwa
ya kazi zake hufanywa na mitambo hivyo kama mwitikio utakuwa mkubwa itasaidia
kuondoa changamoto ya ukosefu wa ajira, tatizo ambalo limekuwa likiwakumba hasa
vijana.
Mkoa wa Ruvuma ni moja kati ya mikoa ambayo imebahatika kuwa
na ardhi nzuri ambayo wananchi wake wamekuwa wakiitumia kwa kuzalisha mazao
mbalimbali ya chakula na biashara, huku changamoto kubwa ikiwa ni kukosekana
kwa viwanda vya usindikaji jambo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo
yao.
Kutokana na serikali ya awamu ya tano kuhamasisha wananchi
wajitokeze kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa, baadhi ya wananchi wameanza
kuitikia mwito huo kwa kasi kubwa ambapo wameweza kujitokeza na kuanzisha
viwanda vidogo vya kusindika nafaka mkoani hapa na hivyo kupelekea wakulima
wapate unafuu kwa njia moja au nyingine, ikiwemo urahisi wa kuuza mazao yao.
Hivi karibuni Mwandishi wetu wa makala haya alipata fursa ya
kutembelea katika mtaa wa Namiholo ambao unajumuisha vitongoji vya Mtakuja, Kambarage,
Soweto, Kisiwani, Miembeni na Mshikamano kijiji cha Peramiho A kata ya
Peramiho, wilayani Songea ambako Kampuni ya Leop and Viann Associates Tanzania
Limited imewekeza kwa kujenga kiwanda kidogo cha kusindika nafaka aina ya
mahindi, jambo ambalo ni faraja kwa wakulima wa maeneo hayo jirani na mkoa wa
Ruvuma kwa ujumla.
Mwenyekiti wa kijiji hicho David Kapinga anasema kwamba, kuanzishwa
kwa kiwanda hicho kutasaidia kuinua uchumi wa wananchi wa Peramiho A, kutokana
na kuwawezesha kuuza mazao yao karibu ambapo kitendo cha mwekezaji huyo kuanza
kununua mahindi kwa ajili ya kiwanda hicho, pia ni mkombozi mkubwa kwa wakulima
wake.
Kapinga anasema kuwa serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula
Taifa (NFRA) Kanda ya Songea mkoani hapa mwaka huu imenunua tani 750 kidogo za
mahindi kwa kata tatu za Peramiho A, Maposeni na Parango hivyo kupelekea
wakulima waliowengi kubaki na mahindi yao majumbani.
“Kwa niaba ya wananchi wangu ninamshukuru mwekezaji huyu kwa
kitendo chake cha kununua mahindi kutoka kwa wakulima tena kwa bei ya shilingi
460 ni msaada mkubwa kwetu, kwani walanguzi wamekuwa wakipita vijijini kununua
kwa bei ndogo ya shilingi 300 hadi 350”, anasema Kapinga.
Anaishauri serikali kuwa na mkakati kabambe wa kuhamasisha
wale wenye uwezo kufikiria kuanzisha viwanda katika maeneo ya vijijini ambako
nako kuna fursa nyingi za kiuchumi, ifanye hivyo ili kuweza kusaidia kuwainua
wakulima ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kuzalisha mazao
mbalimbali huku wakishindwa kunufaika nayo kutokana na kukosa kwa kwenda
kuyauza.
Mkulima Joseph Nyoni anapongeza kitendo cha mwekezaji wa
kiwanda hicho kidogo cha kusindika nafaka kununua mahindi yao kwa kutumia
kipimo cha elektroniki, ikilinganishwa na wanunuzi waliowengi ambao wamekuwa
wakitumia vipimo ambavyo hulenga kumwibia mkulima kwani huvichezea kila wakati
tofauti na hicho cha kisasa ambacho ni vigumu kumwibia mkulima.
Nyoni anabainisha kuwa serikali inaowajibu mkubwa wa
kuhakikisha kwamba kipimo kama hicho ambacho hutumiwa na mwekezaji wa kiwanda
hicho cha Leop and Viann Asosociates Tanzania Limited, kinatumiwa pia na
wanunuzi wengine ili kumnufaisha mkulima ambaye kimsingi ndiye mvuja jasho.
Wakulima Consolata Mwanja, Flora Ndimbo na Adelphina Haulle
wanafafanua kuwa kitendo cha serikali kuhamasisha wawekezaji kuwekeza kwa
kuanzisha viwanda vidogo vidogo ikiwemo vya kusindika nafaka kumetoa fursa kwa
wakulima hasa wadogo, kunufaika kutokana na urahisi wa kuuza mazao yao kwa bei
nzuri ikilinganishwa na hapo awali ambapo wafanyabiashara walanguzi walikuwa
wakipita kuwarubuni majumbani kwao wawauzie kwa bei ya chini huku wao wenyewe wakinufaika
kwa kuuza kwa bei ya juu.
“Mwaka huu tutaongeza uzalishaji wa zao hili la mahindi
kutokana na kuwa na uhakika wa soko la kuuzia ambalo lipo hapa hapa kijijini
kwetu, ikilinganishwa na hapo awali wanunuzi tulikuwa tukitegemea watoke
mijini”, wanasema.
Severine Haulle anaeleza kuwa uwepo wa kiwanda hicho cha
kusindika nafaka za mahindi katika kata ya Peramiho, kumesaidia pia kuhamasisha
wakulima wakipende kilimo cha zao hilo ambapo sasa kuanzia msimu ujao wa kilimo
wengi wao watazalisha kwa wingi zao hilo la chakula na biashara na kwamba
anamwomba mwekezaji wa kiwanda hicho kuanza kununua mapema msimu ujao ili
wakulima waweze kunufaika na bei nzuri wanayonunua.
Haulle anaeleza kuwa wamechoka kuibiwa mazao yao na wanunuzi
ambao kwa miaka mingi wamekuwa kikwazo kwao katika kukabiliana na umaskini wa
kipato hivyo kitendo cha kiwanda hicho kujengwa karibu nao kutasaidia wajikwamue
kiuchumi ikilinganishwa na hapo awali.
Diwani wa kata ya Peramiho, Issack Mwimba anasema kuwa
kiwanda hicho kidogo cha kusindika nafaka kimekuja wakati muafaka ambapo jukumu
la viongozi ni kuhakikisha wanahamasisha wananchi, wajikite zaidi katika
uzalishaji wa mazao hayo kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili wapate mazao
yenye ubora unaohitajika.
Mwimba anafafanua kuwa anauhakika kwamba, uwepo wa kiwanda
hicho chenye dhamira ya kusindika mahindi katika kata yake kitaweza kubadilisha
maisha ya wananchi anaowaongoza, hususan wale ambao watajikita na uzalishaji wa
zao hilo la mahindi na kwamba anamtaka mwekezaji huyo msimu ujao ajitahidi
kufungua soko la ununuzi wa mahindi mapema ili kuweza kuwakomesha wanunuzi
wenye tabia ya kuwaibia wakulima.
Anasema kiwanda hicho kitasaidia kutoa ajira kwa wananchi
wake hivyo anamtaka mwekezaji kuwapa kipaumbele wananchi wa kata hiyo na kwamba
vijana wanapaswa kujiunga na vyuo vya ufundi vya VETA, ili waweze kupata ujuzi
ambao utawawezesha kupata ajira katika viwanda vinavyoanzishwa kwenye maeneo
yao kwani bila kufanya hivyo watashuhudia wakipata ajira watu wa mbali na kuzua
malalamiko yasiyo na maana.
“Ni wazi kuwa uanzishwaji wa kiwanda hiki utapunguza
changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na hivyo kukuza uchumi, sio tu kwa
wananchi wa kata hii na jirani bali pia hata kwa taifa letu kwa ujumla”, anasema
Mwimba.
Diwani huyo pia anasisitiza juu ya wakulima kuacha tabia ya
kuuza mazao yote bila kujiwekea akiba ya kutosha ya chakula na kwamba anawaasa
wataalamu wa kilimo katika kata hiyo ya Peramiho, kuhakikisha wanapita kwa
wakulima kutoa elimu ya namna bora ya uandaaji wa mashamba kwa ajili ya msimu
ujao wa kilimo ili waweze kuzalisha mazao mengi zaidi na yenye ubora kwani
msimu wa kilimo umekaribia kuanza.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama
anasema serikali inadhamini sekta binafsi hivyo kuanzishwa kwa kiwanda hicho
inaonesha jinsi gani Watanzania wazalendo, wanavyounga mkono juhudi za Rais Dkt.
John Magufuli za kuhakikisha kwamba nchi inakuwa ya viwanda na hivyo kusaidia
kukuza uchumi wa taifa.
Jenista ambaye pia ni Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu anapongeza kazi ambayo imeonyeshwa
na mwekezaji wa kiwanda hicho jimboni kwake.
“Kwa niaba ya serikali nishukuru wale waliowaza kuanzisha
kiwanda hiki hapa, kwa kweli kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wangu wa
Peramiho lakini pia niwaombe watu wengine kujitokeza kuwekeza ndani ya mkoa wa Ruvuma
na maeneo mengine ya nchi hii, ili dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya
kuifanya nchi kuwa ya viwanda iweze kutimia kwa manufaa ya wananchi wote”,
anasema.
Anawaasa wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho kujenga
ushirikiano mzuri na mwekezaji huyo ili kuondokana na migogoro ambayo mara
nyingi imekuwa ikijitokeza pindi mtu anapowekeza na kwamba alilitaka Shirika la
Umeme nchini (TANESCO) kuhakikisha linaharakisha kupeleka umeme katika eneo hilo
la kiwanda ili kiweze kuanza kazi kwa wakati na hivyo kunufaisha wananchi
hususani wale ambao watapata ajira.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Viann Komba anasema lengo hasa
la uanzishwaji wake ni kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano
ambayo imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda vikiwemo vidogo na kwamba
waliamua kuanzisha katika eneo hilo la kijijini ili kuongeza fursa kwa wananchi
wa vijiji vinne vya Lundusi, Peramiho A, Peramiho B na Nguvu moja kuwaondolea
changamoto ya kukosa masoko ya mazao wanayozalisha.
Komba anafafanua kuwa anauhakika mradi huo kwa kiasi kikubwa
utasaidia kuinua uchumi wa wananchi ambapo kiwanda hicho kinao uwezo wa kukoboa
na kusaga magunia 200 ya mahindi kwa siku.
Anaeleza kuwa kiwanda hicho cha kusindika nafaka za mahindi
kitakuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi 30 wa kudumu na kwamba wafanyakazi wa
muda ambao watakuwa wakifanya kazi kila siku watakuwa 70 na hivyo kufanya kuwa
na jumla ya wafanyakazi 100.
Akizungumzia kuhusu kipimo kinachotumika kupimia mahindi
yanayoletwa na wakulima kiwandani hapo kwa ajili ya kuuza anasema wameamua kutumia
kipimo cha kielektroniki kutokana na ukweli kwamba, kinawatendea haki wakulima
ikilinganishwa na vipimo vingine ambavyo ni rahisi kuvichezea ili kumpunja
mkulima.
“Sisi hatujaanzisha kiwanda hiki kwa lengo la kumwibia
mkulima bali kujenga urafiki naye kwa kununua mazao anayozalisha kwa bei nzuri,
ili naye hatimaye aweze kujikwamua kiuchumi na sio vinginevyo lakini pia
niwaombe wananchi wanaozunguka kiwanda hiki, wazalishe mahindi yenye ubora ili
wanufaike na bei kubwa”, anasisitiza.
Komba anaeleza kuwa dhamira ya serikali ya kuhamasisha
wananchi wazalendo wajitokeze kuanzisha viwanda vidogo ikiwemo maeneo ya
vijijini ni kutaka mkulima anufaike kwanza kwa kuuza mazao yake kwa urahisi na bei
nzuri lakini pia kuongeza thamani ya mazao hayo kwa njia ya usindikaji.
Pamoja na mambo mengine changamoto kubwa inayowakabili katika
eneo palipojengwa kiwanda hicho, ni kutokuwepo kwa umeme wa uhakika hivyo Shirika
la Umeme nchini (TANESCO) mkoani Ruvuma linaombwa kuharakisha zoezi la
upelekaji wa nishati hiyo, ili kiweze kuanza kazi mara moja kama
ilivyokusudiwa.
Kuanzishwa kwa kiwanda cha kusindika nafaka cha Leop and
Viann Associates Tanzania Limited chenye uwezo wa kusaga tani 15 kwa siku,
kutasaidia kupunguza changamoto ya soko la mahindi lililopo mkoani Ruvuma ambapo
katika kipindi cha mwaka huu, ulikadiria kuzalisha tani 840,000 za mahindi
ambapo Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) Kanda ya Songea katika
kipindi hicho amenunua tani 22,000 na kwamba kati ya hizo tani 840,000 nusu
yake zimebaki majumbani kwa wakulima kwa ajili ya chakula.
Serikali kwa nchi nzima imekadiria kununua tani laki moja za
mahindi pekee, hivyo ni wazi kuwa wakulima watabaki na mahindi mengi majumbani
kwao na kulazimika kutafuta soko maeneo mengine, ambako huko ndiko watakakokutana
na wanunuzi walanguzi ambao hununua kwa bei ya chini.
No comments:
Post a Comment