Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya Wananchi wa kata ya Mkumbi wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, wamesema kwamba hawana imani na diwani wao wa kata hiyo, Thomas Kapinga
kutokana na diwani huyo kudaiwa kuvamia eneo la kituo cha afya cha kata hiyo na
kufanya shughuli za ujenzi wa nyumba yake binafsi.
Aidha walisema kuwa diwani huyo anafahamu kuwa eneo hilo lilitolewa
na Wazee wa kata hiyo tokea miaka 1970 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo
cha afya ikiwemo nyumba za kuishi watumishi, lakini wanamshangaa leo ameibuka
na kudai kuwa ni la kwake na kuanza kufanya shughuli hizo za ujenzi.
Hayo yalisemwa na wananchi hao kwa nyakati tofauti walipokuwa
wakizungumza na waandishi wa habari, ambao walitembelea katika kata hiyo kujionea
maendeleo ya kituo cha afya kata ya Mkumbi.
Kufuatia hali hiyo wananchi hao wameutaka uongozi wa wilaya
hiyo kuingilia kati na kuona namna ya kumaliza mgogoro huo, ambao sasa umedumu
kwa muda mrefu bila kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mwenyekiti wa baraza la Wazee kata ya Mkumbi, Gaufrid
Mazungumzo alisema kuwa wao hivi sasa hawaoni sababu ya kuongozwa na diwani
ambaye hapendi kusikiliza mawazo ya wananchi wake ya kimaendeleo, kwani wao
walitoa eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja na nusu kwa ajili ya
kupanua ujenzi huo wa kituo cha afya.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Mkumbi, Benuard Komba
alifafanua kuwa kitendo cha diwani wao Kapinga kuonesha waziwazi vitendo vya kupingana
na wananchi wake ni dhahiri ameshindwa kuongoza kata hiyo, hivyo wamemtaka
ajiondoe mapema yeye mwenyewe katika nafasi hiyo kabla hawajachukua hatua ya
kumtaka aachie ngazi.
“Ninataka kusema hivi katika eneo hili analogombea na
wananchi sio la kwake, sisi wananchi ndiyo tulilitoa kwa ajili ya matumizi ya
kijamii na sio kwa matumizi ya mtu binafsi, kwa ajumla serikali ya kijiji chetu
haikubaliani na vurugu hizi za diwani huyu”, alisema Komba.
Vilevile Christopher Kongalipongo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) tawi la Mkumbi aliongeza kuwa wanamshangaa diwani Kapinga
waliyemchagua awaongoze kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye, amekuwa wa
kwanza kupinga maendeleo ya wananchi wake na kutengeneza migogoro ya ardhi
isiyokuwa na tija.
“Wazee wa kata hii ya Mkumbi tunaomba kilio chetu kimfikie
Rais John Magufuli ambaye ndiye Mwenyekiti wetu wa Chama, achukue hatua dhidi
ya diwani huyu ambaye anatunyanyasa tumechoka kuvumulia upuuzi huu”, alisema
Kongalipongo.
Alipoulizwa diwani wa kata ya Mkumbi, Kapinga alikiri kuwepo
kwa mgogoro huo kati yake na wananchi hao na kueleza kuwa eneo lenye mgogoro ni
mali yake na yeye anawashangaa wananchi wa kata hiyo, wakisema kuwa lilitengwa
kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kijamii.
Hata hivyo Kapinga alisema kuwa eneo hilo ni mali yake na
ndugu zake, hivyo hawezi kuliacha likapotea kienyeji vinginevyo wamlipe fidia kwanza
endapo kama kuna mtu analihitaji kufanyia shughuli yoyote ya kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment