Mbinga.
WADAU wa elimu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa
kuendelea kuchangia katika sekta ya elimu wilayani humo ili watoto wanapokuwa
shuleni waweze kusoma wakiwa katika mazingira mazuri na kufanya vyema katika
masomo yao.
Aidha taasisi mbalimbali nazo zimetakiwa kuhamasika kuchangia
madawati shuleni na sio kuiachia serikali peke yake, kwani sekta ya elimu ili
iweze kusonga mbele inahitaji mchango kutoka kwa wadau mbalimbali.
Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga Gilbert Simiya alisema hayo
juzi mjini hapa alipokuwa katika zoezi la kukabidhi madawati 80 kwa uongozi wa
halmashauri ya wilaya hiyo, ambayo yalitolewa na Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) ikiwa ni mchango wa madawati hayo uliotolewa kwa ajili ya
matumizi ya watoto wa shule za msingi wilayani hapa.
Simiya alikuwa akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas
Nshenye ambapo alitoa pongezi kwa Wakala huyo kwa kuunga mkono juhudi za Rais
John Magufuli kutoa mchango huo wa madawati ili kusaidia kuboresha sekta hiyo
ya elimu.
“Mchango huu utasaidia watoto wetu kukaa katika mazingira
mazuri ya kusomea natoa pongezi kwa watumishi wa TFS kwa kufanya jitihada ya
kutengeneza madawati haya, natoa wito kwa taasisi zingine nazo zihamasike
kuchangia katika sekta hii ya elimu hapa Mbinga”, alisema.
Awali akitoa taarifa ya Wakala wa huduma za misitu Tanzania,
Meneja wa TFS wilayani Mbinga Festo Chaula alisema kuwa wametoa mchango wa
madawati hayo kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata mafunzo katika mazingira
mazuri shuleni.
Alisema kuwa mojawapo ya malengo ya mpango mkakati wa TFS ni
kuboresha rasilimali hizo na mfumo wa ikolojia (Forest and bee resource base
and ecosystem improved) ambapo kuna dhima ya uwezeshaji jamii kwa kutoa
ushiriki mpana wa wananchi katika kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa na
kutumiwa kwa manufaa ya jamii.
Pamoja na mambo mengine kwa upande wake Ofisa elimu msingi wa
wilaya hiyo, Samwel Komba alitoa shukrani kwa msaada wa madawati waliyoyapata
kutoka kwa Wakala huyo wa misitu Tanzania, huku akieleza kuwa yataweza kusaidia
kukalia watoto 240 watakao kuwa darasani wakati wa masomo.
Hata hivyo wilaya ya Mbinga hivi sasa haina upungufu wa
madawati ya kukalia wanafunzi shuleni ambapo imeweza kuvuka lengo kwa
kutengeneza madawati 19,572 huku mahitaji halisi yakiwa ni madawati 19,421.
No comments:
Post a Comment