Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa tatizo la kulala wanafunzi wawili kitanda
kimoja katika bweni la shule ya Sekondari wasichana Mbinga iliyopo mkoani
Ruvuma, inatokana na upungufu mkubwa uliopo wa majengo na vyumba vya kulala watoto
hao katika shule hiyo, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua za
haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith
Mahenge ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha kwamba unatenga fedha kupitia
vyanzo vyake vya mapato ya ndani, kwa ajili ya kuweza kuanza taratibu za ujenzi
wa bweni hilo la kulala watoto hao ili waweze kuondokana na adha hiyo
wanayoipata sasa.
Dkt. Mahenge alitoa agizo hilo hivi karibuni alipokuwa katika ziara
yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoani hapa, kukagua maendeleo ya shule za
sekondari kwa lengo pia la kujionea changamoto mbalimbali zilizopo kwenye shule
hizo na kuzitafutia ufumbuzi wake.
“Nimegundua hapa kuna tatizo kubwa la upungufu wa vyumba vya
kulala watoto hawa, nauagiza uongozi wa wilaya uone namna ya kutafuta fedha
kupitia mapato yenu ya ndani ili kuweza kumaliza tatizo hili mapema la ujenzi
wa bweni jipya la kulala hawa wanafunzi”, alisisitiza.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa alipozungumza na wanafunzi wa shule
hiyo ambayo ni ya mchepuo wa masomo ya sayansi inayojumuisha watoto wa kike tu,
aliwataka watoto hao kusoma kwa bidii ili serikali hapo baadaye iweze kuwapata
wataalamu wa kutosha katika fani ya masomo hayo.
Alibainisha kuwa kitakachoweza kuwakomboa wananchi wa bara la
Africa katika kuondokana na umaskini ni sisi wenyewe kuweka jitihada katika
kuzingatia suala la elimu, kwa wazazi kupeleka watoto wao shule na kusoma kwa
juhudi na maarifa ili kuweza kusonga mbele kimaendeleo.
Kwa upande wake akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya shule ya
sekondari ya wasichana Mbinga, Makamu mkuu wa shule hiyo Rehema Rohomoja
alimweleza Dkt. Mahenge kuwa halmashauri ya wilaya Mbinga tayari imetenga fedha
shilingi milioni 160.5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya kulala watoto hao.
Rohomoja aliongeza kuwa ujenzi huo wa bweni jipya unatarajiwa
kuanza mapema kuanzia sasa, baada ya taratibu za mchakato wa kumpata mkandarasi
husika na mwenye sifa kukamilika kwake.
No comments:
Post a Comment