Kahawa iliyosindikwa yenye jina maarufu Mbinga Cafe ni sehemu ya bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEBAINISHWA kuwa uzalishaji mdogo wa kahawa ya maganda katika
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma na ongezeko la ushindani katika biashara ya
ukoboaji wa kahawa ni changamoto kubwa inayokikabili Kiwanda cha Kukoboa Kahawa
Mbinga (MCCCO) kwani kimekuwa kikipokea zao hilo kiasi kidogo tofauti na uwezo
mkubwa ilionao wa kukoboa kahawa.
Pamoja na Kiwanda hicho kujengwa kuwa na uwezo mkubwa wa
kukoboa kahawa zaidi ya tani 30,000 kwa mwaka, bado uzalishaji wa za hilo
wilayani humo umekuwa ni mdogo kutoka kwa wakulima ambapo kwa mwaka wamekuwa
wakizalisha tani 5,000 hadi 17,500 tu hali ambayo imekuwa ikisababisha
kushindwa kufikia malengo husika.
Aidha kwa upande wa ushindani wa biashara ya ukoboaji kahawa
umeongezeka kutokana na mji wa Mbinga peke yake hivi sasa, kuna viwanda vitatu
vya kukoboa zao hilo hivyo kutokana na uzalishaji kuwa kidogo kutoka kwa
mkulima, kahawa inayozalishwa imekuwa ni ya mtindo wa kunyang’anyana.
Hayo yalisemwa na Meneja Mkuu wa kiwanda cha kukoboa kahawa
wilayani Mbinga, Jonas Mbunda alipokuwa akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya
kiwanda hicho kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge aliyetembelea juzi kujionea maendeleo mbalimbali kiwandani hapo.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa pamoja na changamoto hizi tulizonazo
hapa wilayani, lakini sisi hapa kwetu kiwandani bado tunaongoza kupokea kahawa nyingi kutoka kwa
mkulima mmoja mmoja na vyama vya ushirika”, alisema Mbunda.
Mbunda alisema kuwa katika msimu wa mwaka huu, MCCCO
wanatarajia kukoboa zaidi ya tani 10,000 na kwamba katika kuongeza mapato ya
kampuni hiyo wamekuwa wakitoa huduma nzuri ya ukoboaji na utunzaji kahawa kwa
vyama vya ushirika, vikundi vya wakulima na wafanyabiashara wenye makampuni
binafsi jambo ambalo huwafanya waweze kukoboa zaidi ya asilimia 60 ya kahawa
inayozalishwa Mbinga.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge
aliwataka wataalamu wa kilimo wa wilaya ya hiyo kwa kushirikiana na Menejimenti
ya Kampuni hiyo ya kukoboa kahawa wilayani hapa, wajenge ushirikiano wa
kuongeza mitambo midogo ya kuchakata kahawa mbivu vijijini ili kuweza kuongeza
ubora wa zao hilo na kuwavutia wakulima wengi kuleta kahawa yao kukoboa katika
kiwanda hicho.
Dkt. Mahenge alisisitiza kuwa lengo kubwa la serikali ni
kuona inaboresha viwanda vyake kwa kuhakikisha kwamba vinafanya kazi
iliyolengwa, ili kuweza kuinua uchumi wa mkulima mwenye kipato cha chini taifa
kwa ujumla kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Hata hivyo Kampuni ya kukoboa kahawa Mbinga inamilikiwa kwa
pamoja kati ya vyama vya ushirika 28 vinavyolima kahawa nchini Tanzania na
serikali kwa ujumla, ambapo vyama vya ushirika vinamiliki asilimia 56.54 ya
hisa zote na serikali asilimia 43.46 ambapo umiliki huo ulianza rasmi Septemba
18 mwaka 1995 wakati kampuni hiyo ilipoanza kubinafsishwa.
No comments:
Post a Comment