Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa mkoa wa
Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amesikitishwa na idadi ya ongezeko la mimba kwa
watoto wa kike wanaosoma shule za sekondari wilayani Mbinga mkoani humo, jambo
ambalo linasababisha washindwe kuendelea na masomo yao.
Dkt. Binilith Mahenge. |
Jumla ya wanafunzi
wa kike 37 wanaosoma katika shule za sekondari zilizopo katika maeneo
mbalimbali wilayani humo wamepewa ujauzito na kesi zao zimefikishwa Polisi, ili
watuhumiwa waliohusika na vitendo vya kukatisha masomo ya watoto hao waweze
kuchukuliwa hatua za kisheria.
Dkt. Mahenge alipokea
taarifa ya kesi hizo ambayo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas
Nshenye juzi alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa, ambapo Mkuu
huyo wa wilaya alisema kuwa mimba hizo wamepewa katika kipindi cha kuanzia
Januari hadi Septemba mwaka huu.
Kufuatia hali hiyo
Mkuu huyo wa mkoa ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha kwamba, suala
hilo linatekelezwa kikamilifu kwa kuhakikisha watuhumiwa wote waliohusika
kufanya vitendo hivyo wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
“Mnasema uchunguzi
bado unaendelea, natoa agizo kwenu viongozi wote wa wilaya hii hakikisheni
jambo hili linafanyiwa kazi haraka na kwa wakati wahusika wa vitendo hivi,
wanakamatwa haraka na kufikishwa kwenye mkono wa sheria”, alisisitiza Dkt. Mahenge.
Awali Mkuu wa
wilaya ya Mbinga, Nshenye alimweleza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge kuwa
kesi hizo za kuwapatia ujauzito watoto hao wa shule za sekondari zimekwama
Polisi na bado hazijafikishwa mahakamani kutokana na jamii kutotoa ushirikiano
wa karibu wakati wa kuwakamata watuhumiwa waliohusika na vitendo hivyo.
"Kwa upande
wa shule za msingi tatizo hili hapa wilayani hakuna, limekuwa likitusumbua hasa
kwa shule za sekondari, wazazi wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha katika
kukabiliana nalo", alisema Nshenye.
Nshenye aliongeza
kuwa uchunguzi juu ya tatizo hilo bado unaendelea ili hatua zaidi ziweze
kuchukuliwa na kuweza kupunguza tatizo hilo, ambalo linakatisha ndoto za
maendeleo ya watoto wa kike katika nyanja ya elimu.
No comments:
Post a Comment