Na Julius Konala,
Songea.
BAADHI ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma wamewalalamikia Wabunge
wa mkoa huo, kwa kushindwa kuwa na umoja katika kupigania suala la shirika la ndege
za serikali (ATC) kutua kwenye uwanja wa Manispaa ya Songea mkoani humo,
wakidai kuwa ni muda mrefu sasa umepita mkoa huo umesahaulika katika masuala ya
usafiri wa anga.
Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wananchi hao walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Songea, ambapo wamedai kuwa
wanashindwa kusafiri mara kwa mara kwa ndege ya Kampuni ya mtu binafsi
inayofanya safari zake jijini Dar es salaam hadi Songea kutokana na gharama
zake kuwa kubwa.
Mmoja wa wakazi wa Manispaa hiyo, Mohamed Abdallah alisema
kuwa wananchi wa mkoa huo wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wa kusafiri kwa
basi hadi mkoa wa Mbeya, kwa ajili ya kufuata huduma ya usafiri wa anga wakati
usafiri huo endapo ungefanya safari zake mkoani humo na kwa bei ndogo
ungesaidia kwa kiasi kikubwa hata kuleta wawekezaji na watalii watakaotembelea
fukwe za ziwa Nyasa na wananchi kusafiri kwa ndege hizo.
“Mategemeo ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma ni kwamba wabunge
wetu wangeweza kupigania ndege hizi zifanye safari zake hadi mkoani hapa, kwa
lengo la kuwapunguzia mzigo wa kusafiri kwa gharama kubwa wananchi wao badala
ya kushughulika kila mmoja na jambo la jimboni kwake”, alisema Abdallah.
Alisema kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo ukosefu wa umeme wa uhakika, jambo ambalo linapaswa kupiganiwa na
wabunge hao katika kuonesha juhudi ya kuharakaisha umeme wa Gridi ya taifa
unaingia mkoani humo badala ya kuona suala hilo kama ni la mtu mmoja.
No comments:
Post a Comment