Thursday, December 1, 2016

MANISPAA YA SONGEA YATEKETEZA BIDHAA FEKI ZENYE VIAMBATA VYA SUMU YENYE MADHARA KWA BINADAMU

Na Kassian Nyandindi,         
Songea.

KATIKA kuhakikisha kwamba udhibiti wa vyakula na dawa unakuwa endelevu katika Manispaa ya Songea mkoa wa Ruvuma, idara ya afya halmashauri ya Manispaa hiyo imefanya ukaguzi wa kushitukiza na kuweza kukamata vyakula vibovu na vipodozi ambavyo vina sumu vyenye thamani ya shilingi 500,000.

Aidha ukaguzi huo wa vyakula ambavyo vimekamatwa na muda wake wa matumizi umepita, viliweza kupatikana vya shilingi 300,000 huku chumvi isiyokuwa na madini joto ikiwa ni ya shilingi 80,000 na vipodozi vyenye viambata vya sumu vikiwa vyenye thamani ya shilingi 120,000.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowafikia waandishi wa habari na kuthibitishwa na Ofisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo ilieleza kuwa watuhumiwa waliokamatwa wakihusika kuuza bidhaa hizo wamechukuliwa hatua ya kulipishwa faini ya shilingi 122,500 kila mmoja ikiwemo na gharama ya uteketezaji.


Midelo alisema kuwa wito umetolewa kwa wafanyabiashara wanaouza vyakula na vipodozi kuacha mara moja tabia ya kuuza bidhaa feki ambazo zimepitwa muda na matumizi yake, ili kuweza kulinda afya za walaji na watumiaji.

Katika hatua nyingine Ofisa habari huyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mnamo Novemba Mosi hadi 20 mwaka huu, jumla ya watu 15 katika Manispaa ya Songea mtaa wa Osterbay kata ya Msamala wameng’atwa na mbwa wanaodaiwa kuwa na kichaa.

Alisema kuwa katika kupambana na hali hiyo wataalamu wa afya na mifugo wanaendelea kutoa chanjo kwa wanyama hao na elimu kwa watu wanaofuga ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo, ambalo linahatarisha usalama wa maisha ya watu katika maeneo yao wanayoishi.


Hata hivyo tayari watu waliojeruhiwa na mbwa hao wamepatiwa tiba na kwamba wafugaji wa mbwa katika Manispaa hiyo, wametakiwa kuwadhiti wanyama hao kwa kuwafungia ndani ya vibanda wasiweze kuzurula hovyo wakati wa mchana na kuleta madhara kwa binadamu.

No comments: