Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani
amezitaka taasisi za kifedha hapa nchini kushirikiana na wawekezaji binafsi
ambao wanazalisha umeme wa nguvu ya maji, katika kuwapatia mikopo yenye riba
nafuu ili waweze kuendesha shughuli ya uzalishaji wa nishati hiyo kwa ufanisi
zaidi.
Dkt. Medard Kalemani. |
Aidha ameeleza kuwa serikali kwa kushirikiana pia na Wakala
wa umeme vijijini (REA) wameweka mikakati ya kuhakikisha kwamba umeme
utapelekwa katika maeneo yote ya vijijini na kwenye taasisi za serikali, kwa
lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo ambayo
hayajafikiwa na umeme.
Hayo yalisemwa na Dkt. Kalemani juzi alipokuwa katika ziara
yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakati alipotembelea kituo cha
kuzalisha umeme wa nguvu ya maji unaoendeshwa na kampuni ya Andoya Hydro
Electric Power(AHEPO) katika kata ya Mbangamao wilayani humo.
“Watanzania wengine waige mfano kama huu, ninawasifu sana
mmeweza kuzalisha umeme huu wa nguvu ya maji megawati 500 na kuweza kuunganisha
na mini gridi ya TANESCO hapa Mbinga pamoja na kuwasambazia wananchi vijiji
jirani ambao sasa wanautumia kwa shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo”,
alisema Dkt. Kalemani.
Awali akitolea maelezo juu ya maendeleo ya mradi huo, Jasper
Bubelwa ambaye ni Injinia mkuu wa mradi wa AHEPO alimweleza Dkt. Kalemani kuwa
hivi sasa kampuni hiyo, inashindwa kufikia malengo husika ya kuendelea kujenga
njia za kusafirisha umeme katika maeneo ya baadhi ya vijiji kutokana na mabenki
ya biashara na taasisi za kifedha kutoza riba kubwa.
Injinia Bubelwa alieleza kuwa pia wanafanya jitihada ya
kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza mashine ya pili yenye uwezo wa kuzalisha
megawati 500 za umeme ili waweze kufikia malengo ya kukamilisha uzalishaji wa
megawati 1 na kuweza kuendelea kuwasambazia wananchi.
Hata hivyo hadi kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya mradi
huo na kusambaza nishati hiyo, jumla ya wateja 922 wanatarajiwa kufikiwa kati
ya 3,835 waliopo katika vijiji vya Lifakara, Kilimani na Mbangamao na ziada ya
nishati ya umeme kuunganishwa kwenye mfumo wa mini gridi ya Shirika la Umeme
Tanzania iliyopo hapa wilayani Mbinga.
No comments:
Post a Comment