Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
JAMII hapa nchini imeshauriwa kuacha kukata miti hovyo na
kuitumia kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, badala yake wanapaswa kutumia
nishati ya makaa ya mawe kwa ajili ya shughuli zao za kila siku, hatua ambayo
itasaidia kutunza mazingira na kuepukana na athari kubwa ya uharibifu wa
mazingira kunakosababishwa na matumizi ya kuni.
Kufuatia hali hiyo serikali kupitia wataalamu wake imeombwa
kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi, juu ya madhara ya ukataji miti na matumizi
ya kuni kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine za kibinadamu.
Makaa ya mawe. |
Ushauri huo ulitolewa juzi na Leah Kayombo ambaye ni Meneja
wa shirika lisilokuwa la kiserikali, Mbalawala Women Group Organisation
lililopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kuona namna shirika hilo,
lilivyofanikiwa katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwenye maeneo
yaliyoathirika zaidi na uchimbaji wa makaa ya mawe kijijini humo.
Kayombo alisema kuwa kutokana na kasi kubwa ya
uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu katika vijiji
vinavyozunguka mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka, kuanzia mwaka 2014 hadi kufikia
mwezi Machi mwaka huu wameweza kupanda miti 36,000 pamoja na kuanzisha vitalu
vya miti ambayo imesambazwa bure katika taasisi za umma kama vile shule,
hospitali na watu binafsi ili nao waweze kuipanda katika maeneo yao.
Alisema kuwa lengo la kuanzisha mradi wa
upandaji na uanzishwaji wa vitalu vya miti ni kuisaidia serikali
katika kupambana na uharibifu wa mazingira, ili watu waweze kuipanda na kuweza
kuhifadhi uoto wake wa asili katika misitu hata kwenye vyanzo vya maji.
Kayombo aliafanua kuwa shirika hilo linaundwa na serikali ya
vijiji vya Ruanda na Ntunduaro kwa kushirikiana na Mwekezaji wa mgodi wa
Tancoal Energy na kwamba, wamekuwa wakijishughulisha na utengenezaji wa makaa
ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani na kuweza kuajiri baadhi ya vijana
ambao wengine wana ajira za muda na kudumu.
Licha ya kupata mafanikio hayo alieleza kuwa bado
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile wateja wa uhakika,
ukosefu wa gari lenye uwezo wa kubeba kiasi kikubwa cha makaa ya
mawe kwenda kwa wateja pamoja na kukosekana kwa huduma ya maji,
jambo ambalo linawafanya kutegemea msaada kutoka kwa mwekezaji wa
mgodi huo ambaye huwasaidia pale wanapokwama jambo fulani.
Kwa mujibu wa Kayombo ni kwamba, wameshaanza kuchukua
hatua ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuanza kuchimba visima virefu
vitakavyosaidia kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.
Hivi sasa kuna baadhi ya watu kutoka katika baadhi ya mikoa
hapa nchini, wameonesha nia ya kuhitaji makaa hayo wanayotengeneza kwa ajili ya
shughuli za kupikia ambapo ni kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Songea pamoja na
wateja kutoka ndani ya wilaya ya Mbinga.
Kwa upande wake Meneja uzalishaji wa kikundi hicho, Hajiri
Kapinga ameishukuru Kampuni ya Tancoal Energy, kwa kuwapatia msaada wa mashine
ya kutengeneza makaa hayo, kujenga maabara ya kufanyia shughuli hizo za
utengenezaji mkaa na mtaalamu aliyebobea katika utengenezaji wa makaa kwa ajili
ya matumizi ya nyumbani.
No comments:
Post a Comment