Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imeanza
mchakato wake wa kuanzisha kituo cha kurusha matangazo (Redio ya jamii) ambayo
itakuwa ikiyarusha ndani ya wilaya hiyo, kwa lengo la kuhamasisha maendeleo mbalimbali
ya wananchi.
Yeremias Ngerangera ambaye ni Ofisa habari wa wilaya hiyo
aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mchakato wa kuanzisha Redio hiyo ya jamii,
unaendelea vizuri ambapo tayari kamati ya kusimamia suala hilo imeundwa na
kuanza kazi yake.
Alitaja idara zilizopo kwenye kamati hiyo ni idara ya
mipango, utawala, maendeleo ya jamii, afya, mazingira pamoja na kitengo cha
sheria na usalama ambazo zinatoka katika halmashauri ya wilaya ya Namtumbo.
Kadhalika alibainisha kuwa sababu za halmashauri hiyo
kuanzisha kituo hicho cha kurusha matangazo ni pamoja na kurahisisha
mawasiliano kati ya uongozi wa halmashauri, wananchi na wilaya kwa ujumla juu
ya maagizo mbalimbali ambayo yanatolewa kwa kuwataka wananchi wake waweze kuyatekeleza.
Pia Redio hiyo itatumika kuelimisha jamii juu ya masuala ya
kuzingatia kilimo bora, umuhimu wa utunzaji wa mazingira, kuhamasisha kupeleka
watoto shule, kuwa na afya bora na mambo mengine ya kimaendeleo.
Naye Kaimu Ofisa mipango wa halmashauri ya wilaya hiyo,
Gwakisa Mwaseba ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia mchakato wa
kuanzisha Redio hiyo, alisema kuwa zaidi ya shilingi milioni 103,400,000
zinahitajika ili kuweza kukamilisha zoezi hilo.
Gwakisa aliongeza kwa kuwataka wadau kutoka sehemu mbalimbali
ndani na nje ya Namtumbo, kushirikiana kwa pamoja katika kuchangia uanzishaji
wake pamoja na maendeleo ya wilaya kwa ujumla.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Christopher Kilungu ameitaka
kamati hiyo iliyoundwa kusimamia kikamilifu zoezi hilo kwa kufanya utekelezaji
husika kwa weledi na kuhakikisha unaleta ufanisi mkubwa, ili wananchi wa
Namtumbo waweze kuwa na Redio yao ya kijamii.
Vilevile wananchi wa wilaya hiyo walipoelezwa kupitia
mikutano ya hadhara juu ya kuanzishwa kwa kituo hicho cha kurusha matangazo, walifurahishwa
na hatua hiyo huku wakisema ni nzuri yenye kuwafanya waweze kusonga mbele
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment