Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao unahudumia kaya
maskini katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, umeengua kaya
hewa 2,692 ambazo zimebainika kwamba hazikuwa na sifa ya kuendelea kupewa
ruzuku ya kuhudumia kaya maskini.
Kaya zilizoenguliwa ni kati ya 7,695 zilizokuwa zinanufaika
na ruzuku hiyo ambapo hivi sasa baada ya uhakiki kufanyika, kaya zenye sifa ya
kupata fedha kutoka kwenye mfuko huo zimebakia 5,003.
Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alibainisha
hayo jana alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kueleza kuwa tayari
shilingi milioni 277 zimetolewa kwa kaya maskini 5,003 zilizopo katika mitaa 53
ya Manispaa ya Songea ambayo ipo kwenye mpango wa kupewa ruzuku.
Vilevile alisema kuwa kaya ambazo zimeondolewa kwenye mpango
huo zimekabidhiwa barua rasmi juu ya kuenguliwa kwao, baada ya uhakiki wa
nyumba kwa nyumba kufanyika ambao ulibaini kaya hizo kutokuwa na sifa.
Midelo aliongeza kuwa kati ya kaya zilizoenguliwa ilibainika
kuwa kaya 1,599 hazikuwa maskini, kaya 342 walihama katika maeneo yao ya awali
waliyokuwa wakiishi, kaya 110 walifariki dunia, kaya 417 zilibainika kuwa ni
hewa na kaya 144 hazikuwepo kwenye uhakiki huo.
Pamoja na mambo mengine halmashauri ya Manispaa ya Songea
imeendelea kupokea fedha kwa ajili ya mpango wa kunusuru kaya maskini kupitia
mradi wa TASAF awamu ya tatu, ikiwa ni lengo la kupunguza umaskini kwa watu
wasiojiweza na kwamba hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni
1.6 zilipokelewa katika Manispaa hiyo.
No comments:
Post a Comment