Baadhi ya Wakazi mji mdogo wa Peramiho mkoani Ruvuma, wakisikiliza kwa makini uzinduzi wa kampeni ya kupunguza na kuzuia udumavu kwa watoto. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
WANANCHI wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa kuwa na
mikakati na mipango thabiti, yenye kulenga kupunguza tatizo la utapia mlo
wilayani humo ambao umekuwa ukiwaathiri watoto wadogo katika makuzi yao, kwa
kuwafanya waonekane kuwa wamedumaa.
Mwito huo umetolewa juzi na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Pendo
Daniel alipokuwa akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Peramiho wilayani hapa
wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupunguza na kuzuia udumavu kwa watoto hao.
Alisema kuwa serikali tayari imekwisha agiza, kutenga na
kuongeza bajeti ya lishe katika ngazi zote ikiwemo shilingi 1,000 kwa kila
mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kwa mwaka na kwamba, maagizo hayo
tayari yametolewa kwenye ngazi husika katika halmashauri zote za mkoa huo.
Alisema kuwa utoaji wa vitamin A pamoja na dawa za kutibu
minyoo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na uwekaji wa madini joto
katika chumvi, nguvu kubwa imekuwa ikitumika katika uhamasishaji na utoaji wa
elimu kwa umma ambapo wilaya ya Songea, shirika lisilokuwa la serikali
Counsenuth hujishughulisha na utoaji huo wa lishe kwa wilaya hiyo na ile ya Madaba
iliyopo mkoani hapa.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa lishe mkoani
Ruvuma wa shirika hilo, Fatuma Hamis alisema kuwa tayari kwa
kushirikiana na serikali wanaendelea kuhamasisha wananchi, kuwapa elimu ya
lishe bora kwa watoto wadogo na hatimaye wameweza kufanikiwa kutokomeza udumavu
huo.
Fatuma alieleza kuwa takwimu za utafiti wa masuala ya lishe
uliofanywa na shirika lake mwaka 2013 katika wilaya ya Songea zinaonesha kuwa
asilimia 37.3 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili ni wadumavu, ambao
wanashindwa kukua na kufikia urefu unaotakiwa kulingana na umri wao.
No comments:
Post a Comment