Na Kassian Nyandindi,
Songea.
IMEELEZWA kuwa jumla ya watu 133 waliokuwa wakiishi katika Halmashauri
ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamefariki dunia katika kipindi cha mwaka 2015
baada ya kuugua ugonjwa hatari wa malaria.
Aidha katika mwaka huo Manispaa hiyo ilikuwa na wagonjwa
28,624 waliougua ugonjwa huo na kutibiwa katika maeneo mbalimbali ya kutolea
huduma za afya, ambao ni sawa na asilimia 16.9 ya wagonjwa wote 169,266.
Ofisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo alisema
hayo jana alipokuwa akihojiwa na mwandishi wa habari hizi na kuongeza kuwa wagonjwa
waliougua na kulazwa katika kipindi hicho walikuwa 8,084 sawa na asilimia 28.8
ya wagonjwa wote 30,129 waliolazwa na kuruhusiwa kurudi makwao.
Kwa mujibu wa Midelo alifafanua pia watoto chini ya miaka
mitano waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo walikuwa 57 ikiwa ni sawa na
asilimia 10, ya vifo vyote vilivyotokea kwa watoto wenye umri chini ya miaka
mitano.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya wagonjwa wa malaria wa nje
katika Manispaa hiyo imepungua toka 63,618 mwaka 2014 hadi wagonjwa 28,624
mwaka 2015 na kwamba idadi ya vifo vilivyotokana na ugonjwa wa malaria vimepungua
kutoka 189 mwaka 2014 hadi vifo 133 mwaka 2015.
Midelo alisema kuwa mikakati mbalimbali iliyowekwa katika kupambana
na tatizo hilo ni kwamba elimu ya afya itaendelea kutolewa kwa jamii ikiwemo
kuharibu mazalia ya mbu, matumizi sahihi ya vyandarua wakati wote wa kulala
pamoja na kupima afya zao ili waweze kupewa matibabu kwa wakati hususani kwa
wale wanaobainika kuwa na vimelea vya wadudu wa ugonjwa huo.
Hata hivyo alieleza kuwa katika kuhakikisha hilo
linatekelezwa na kuleta ufanisi mkubwa, mwaka 2015 halmashauri ya Manispaa ya
Songea ilipata vyandarua 29,125 ambavyo viligawiwa kwa wanafunzi wa shule za
msingi na kwamba katika kipindi cha mwaka huu, halmashauri pia ilipokea
vyandarua 36,020 na kuvigawa kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo.
No comments:
Post a Comment