Ofisi kuu za Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imefanikiwa
kukusanya mapato kutoka katika vyanzo vyake vya ndani kiasi cha zaidi ya shilingi
bilioni 1.1 katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Disemba mwaka huu.
Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kwamba katika
kipindi cha mwaka huu wa fedha Manispaa hiyo inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi
bilioni 3.3.
Midelo alifafanua kuwa makusanyo hayo ni sawa na asilimia
33.27 na kwamba lengo la kufikia asilimia 100 ya makusanyo linatarajiwa kufikia
kabla ya mwishoni mwa mwaka wa fedha Juni 30, 2017.
Alisema kuwa Manispaa ya Songea imekuwa ikipiga hatua kubwa
katika ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kila mwaka, ambapo kwa miaka mitano
iliyopita halmashauri ilifanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 521.09 kutoka
mwaka wa fedha 2011/2012 hadi 2015/2016.
Aliongeza kuwa halmashauri hiyo ya Manispaa imefanikiwa pia kukusanya
mapato ya ndani kupitia matumizi ya mfumo wa kieletroniki katika ukusanyaji wake
(The Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS) ambao una
uwezo wa kuunganishwa na watoa huduma wengine kama vile benki na kampuni ya simu
za mkononi katika kurahisisha malipo ya tozo za serikali.
Kwa mujibu wa Ofisa habari huyo, mfumo mwingine ambao
umesaidia kuongeza ukusanyaji mapato ya ndani ni matumizi mazuri ya mashine za
kieletroniki aina ya Point Of sale (POS) zinatumika katika ukusanyaji wa mapato
hayo na kutoa stakabadhi kwa mlipaji wa huduma au tozo, badala vitabu vya
kawaida vilivyokuwa vinatumika hapo awali.
Alibainisha kuwa mashine hizo zimeunganishwa na mfumo wa
mapato wa LGRCIS ambapo mkusanyaji wa mapato na makusanyo yake hufahamika hata
kama hajafika kuwasilisha sehemu husika.
Hata hivyo halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya mashine
aina ya POS 30 ambazo zinatumika kukusanya mapato katika vyanzo vyake mbalimbali
ikiwemo masoko, maegesho ya magari, Stendi za kubeba abiria, machinjio na
ushuru wa mazao ya misitu na nafaka.
No comments:
Post a Comment