Saturday, December 24, 2016

WATU WENYE UKIMWI MBINGA WATAKIWA KUZINGATIA DAWA

Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

MRATIBU wa kudhibiti na kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Francis Kapinga amewataka watu ambao wamepima afya zao na kubainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo wilayani humo kuzingatia ratiba ya kunywa dawa kwa wakati na sio kuzembea, hali ambayo amesema kuwa endapo wasipozingatia hilo wanaweza kuhatarisha usalama wa afya zao.

Aidha Kapinga amefafanua kuwa wengi wao hivi sasa wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo wamekuwa watoro wa kuzingatia ratiba ya kunywa dawa kwa wakati na kwamba, jitihada zinaendelea kufanyika kuwatafuta pale walipo ili waweze kuendelea kunywa dawa hizo.

Kadhalika alibainisha kuwa upimaji na ushauri uliotolewa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 51,639 wakiwemo wanawake 26,421 na wanaume 25,218 walijitokeza kupima afya zao.


Alifafanua kuwa waliogundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo ni 1,126 ambapo katika kipindi hicho wanawake walikuwa 641 na wanaume 485 sawa na asilimia 2.2.

“Hivyo ndivyo inavyoonesha hali halisi ya kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huu wa Ukimwi ambapo katika mwaka 2015 tulikuwa na maambukizi yenye kufikia asilimia 3.4 na sasa katika kipindi cha mwaka huu ni asilimia 2.2 tu”, alisema Kapinga.


Pia aliongeza kuwa dawa za kufubaza Virusi Vya Ukimwi (VVU) zinapatikana wakati wote kwa wateja husika bila kupungukiwa, hivyo watendaji wa kitengo hicho cha kupambana na ugonjwa huo wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ili kuweza kudhibiti maambukizi mapya yasiendelee kutokea.

No comments: