Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inatarajia
kutumia shilingi milioni 488 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika mtaa
wa Ruhuwiko Kanisani, kwa lengo la kuwaondolea kero upatikanaji wa maji wakazi
wanaoishi katika mtaa huo.
Aidha tayari Manispaa hiyo imeingia mkataba na kampuni ya
Giraf Investment na kwamba hadi sasa mradi huo, ambao umefadhiliwa na benki ya
dunia ujenzi wake umefikia asilimia 95.
Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alisema
hayo alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari mjini hapa, huku akiongeza kuwa
ni asilimia ndogo imebakia katika kukamilisha ujenzi wake ili wananchi hao waweze
kukabidhiwa mradi na kuanza kuutumia.
“Idara ya maji tayari imefanya mkutano wa hadhara na wakazi
wa mtaa huu juu ya taratibu za watumiaji maji na namna ya kuchangia, ili mradi
uweze kuwa endelevu”, alisema Midelo.
Midelo alisema kuwa mradi pia unatumia nguvu ya umeme
kupandisha maji kwenye tanki kubwa hivyo watumiaji wa maji wanatakiwa kuchangia
gharama kidogo kila mwishoni mwa mwezi na kwamba, lengo la idara hiyo katika Manispaa
ya Songea ni kuukabidhi mradi katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa mazingira
(SOUWASA) ambao watasimamia uendeshaji wake.
Wakati huo huo idara hiyo ya maji katika Manispaa hiyo
imekamilisha ukarabati wa visima viwili ambavyo vinatarajia kuhudumia watu
zaidi ya 500 vilivyopo katika shule ya sekondari Mdandamo, iliyopo kata ya
Mletele ambacho kimegharimu shilingi milioni 2.2 na kingine kilichopo shule ya
msingi Luhira katika kata ya Mshangano kilichogharimu shilingi milioni 2.8.
No comments:
Post a Comment