Na Gideon
Mwakanosya,
Songea.
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka Novatus Luambano (32)
mkazi wa kijiji cha Mahanje Madaba wilayani songea, ambaye ni
dereva wa basi dogo ambalo liliacha njia kisha kupinduka na
kusababisha kifo cha abiria mmoja na wengine 27 kujeruhiwa vibaya.
Zubery Mwombeji Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma. |
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewaambia
waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 15 mwaka huu, majira ya
mchana huko katika kijiji cha Hanga Ngadinda wilaya ya Songea vijijini
ambapo gari lenye namba za usajili T 435 BHT aina ya Toyota Coster, lililokuwa
likiendeshwa na Novatus lilipinduka kutokana na kuwa katika mwendo kasi kisha
dereva huyo kutokomea kusikojulikana.
Alimtaja aliyefariki dunia papo hapo katika ajali hiyo kuwa ni
Witness Tembe (11) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Matarawe iliyopo
katika Manispaa ya Songea mkoani hapa.
Katika ajali hiyo alieleza kuwa watu 27 walijeruhiwa vibaya
ambapo kati yao 17 walitibiwa na kuruhusiwa kurudi majumbani kwao na wengine
hali zao ni mbaya bado wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma kwa matibabu
zaidi.
Aliwataja waliolazwa kuwa ni Emilia Haule (21) mkazi wa
Njombe mjini, Madia Ally (1), Sailisi Ndunguru (29) na Viligilia Mkinga (52)
wote wakazi wa Mjimwema Manispaa ya Songea, Sheiba Hussein (28), Michael
Ndunguru (31) na Rajabu Athuman (40) wote wakazi wa kijiji cha Likarangilo nje
kidogo ya Manispaa hiyo na kwamba Alatanga Mdowe (45) mkazi wa mji mdogo wa Madaba,
Beatrice Nchimbi (29) mkazi wa Mahanje huku majeruhi mmoja ambaye ni
wa jinsia ya kiume hakuweza kutambulika majina yake kutokana na hali yake kuwa
mbaya akishindwa kuzungumza.
No comments:
Post a Comment