Julius Konala,
Songea.
BARAZA maalum la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma, limewasimamisha kazi kwa muda usiojulikana watumishi wake watatu
wa halmashauri hiyo kwa ajili ya kupisha uchunguzi, dhidi ya tuhuma
zinazowakabili za kubadili matumizi ya fedha bila kupewa idhini na kamati ya
fedha, uchumi na mipango.
Watumishi hao wamesimamishwa juzi katika kikao maalum cha
baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mjini hapa, chini ya
Mwenyekiti wake Rajab Mtiula na kuhudhuriwa na sekretarieti ya mkoa huo pamoja
na wakuu mbalimbali wa idara wa wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rajab Mtiula aliwataja
watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni Wenisalia Swai ambaye ni Ofisa maendeleo
ya jamii, Mwajuma Sekelela mweka hazina na Amina Njogela Ofisa ugavi na
manunuzi wote wa halmashauri ya wilaya ya Songea.
Mtiula alifafanua kuwa Wenisalia Swai amesimamishwa kazi kutokana
na kuidhinisha fedha kinyume na miongozo husika ambazo zilikuwa zimepokelewa
kwa ajili ya ukarabati wa kituo cha afya Mhukuru, wakati alipokaimu nafasi ya Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri hiyo kwa lengo la kumlipa mkandarasi aliyejenga jengo la
makao makuu ya halmashauri hiyo.
Kadhalika Mwajuma Sekelela naye amesimamishwa kutokana na kosa
la kushindwa kumshauri Kaimu mkurugenzi wa wakati huo asifanye hivyo, huku
Amina Njogela ambaye alikuwa Ofisa ugavi na manunuzi amesimamishwa kwa kosa la
kuchelewesha zabuni ya mradi wa umwagiliaji.
Alisema kuwa sababu nyingine iliyopelekea wasimamishwe kazi
ni kutumia fedha za utekelezaji wa mradi wa skimu hiyo ya umwagiliaji, kumlipa
mkandarasi aliyejenga jengo la makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya
ya Songea Simoni Bulenganija alisema kuwa atahakikisha anafuata taratibu, kanuni
na sheria za utumishi wa umma katika kuwachukulia hatua za kinidhamu bila ya
kumuonea mtumishi yeyote.
Hata hivyo baraza hilo la madiwani limeazimia pia kuunda timu
kwa ajili ya uchunguzi zaidi, kwa lengo la kubaini kama kuna ubadhirifu wowote
wa fedha za miradi ya wananchi ndani ya halmashauri hiyo ili wahusika
wachukuliwe hatua za kinidhamu ikiwa pamoja na kuwafikisha mahakamani.
No comments:
Post a Comment