Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imejiwekea
mkakati wa kupanga na kupima maeneo yote ya bonde la Hagati na tarafa ya Mbuji
yaliyopo wilayani humo, kutokana na wakazi wanaoishi katika maeneo hayo
kuendeleza maeneo yao kwa kujenga makazi holela.
Aidha imeelezwa kuwa sababu nyingine inayoifanya halmashauri
hiyo kutaka kutekeleza mpango huo ni ongezeko kubwa la idadi ya watu wanaoishi
katika maeneo hayo, huku ardhi iliyopo haitoshelezi kwa matumizi ya binadamu na
asilimia kubwa wananchi wake wamekuwa wakitumia maeneo yao kwa shughuli za
kilimo cha zao la kahawa.
Vilevile imefafanuliwa kuwa maeneo ya bonde hilo la Hagati na
tarafa ya Mbuji hayana mgawanyiko rasmi wa matumizi ya ardhi hivyo halmashauri
hiyo ya wilaya ya Mbinga, inakusudia kupanga na kupima maeneo ya wananchi bila
kuathiri hali halisi ya mazingira yaliyopo sasa kwa kuzingatia kanuni na
taratibu za sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 pamoja na sheria ya mipango
miji namba 7 ya mwaka 2007.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Gombo
Samandito alisema hayo juzi alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi juu ya
mapendekezo ya upangaji ardhi katika maeneo hayo, kwa lengo la kuondoa ugumu wa
kusambaza huduma za kijamii kwa wananchi hao kama vile huduma ya ujenzi wa
miundombinu ya barabara, maji, zahanati na shule ili kuweza kumfikia kila
mwananchi katika eneo husika.
Samandito alisema kuwa eneo kubwa la bonde la Hagati na
tarafa ya Mbuji limekuwa likitumika kwa shughuli hizo za kilimo na kusababisha
upungufu mkubwa wa maeneo ya matumizi mengine ya huduma za kijamii kama vile
ujenzi wa masoko, viwanda vidogo vidogo, maeneo ya wazi na yale ya kufanyia
biashara.
“Kukua na kuongezeka kwa uhitaji wa makazi ya wananchi katika
maeneo haya pamoja na eneo kubwa la ardhi kupandwa zao la kudumu la kahawa
kumepelekea tuwe na ongezeko kubwa la ujenzi usio rasmi, yaani makazi holela
ambayo kwa namna moja au nyingine yameongeza kasi ya matumizi ya ardhi hivyo ni
lazima tupange miji yetu kwa utaratibu unaotakiwa ili tuweze kunusuru hali hii kwa
faida ya kizazi cha sasa na baadaye’, alisisitiza Samandito.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa upimaji huo wa ardhi
utakapokamilika mwananchi anayemiliki kipande chake cha ardhi baada ya kupimwa,
atapewa hati miliki huku akifafanua kuwa ekari moja itakuwa ikipimwa kwa
gharama ya shilingi 100,000 ambayo mwananchi huyo atapaswa kulipia.
Kwa upande wao wananchi wanaoishi katika maeneo ya bonde la
Hagati na tarafa ya Mbuji wilayani hapa, waliupokea mpango huo kwa mikono
miwili huku wakisema kwa nyakati tofauti kuwa hawawezi kuukataa kwani ni jambo
muhimu kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo walisema kuwa upimaji huo utaweza kusaidia pia
kuzuia kuzuka kwa migogoro ya ardhi kiholela, ambayo inasababishwa na tatizo la
kutokuwepo kwa mipaka inayotambulika kisheria na kuikosesha pia serikali mapato
yake yanayotokana na kodi ya ardhi ambayo mara nyingi hutolewa kwa
uthaminishaji wa maeneo yaliyopimwa.
No comments:
Post a Comment