Tuesday, December 27, 2016

MBINGA WAVUKA LENGO UTOAJI CHANJO KWA WATOTO WADOGO

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IDARA ya afya kupitia kitengo chake cha huduma ya afya, uzazi na mtoto katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kimeweza kuvuka lengo la kitaifa kwa kutoa chanjo watoto 14,436 sawa na asilimia 98.7 ya waliochanjwa chanjo za kuzuia magonjwa ya aina mbalimbali wilayani humo.

Watoto waliochanjwa ni wale wenye umri wa mwaka mmoja na kwamba kuna jumla ya chanjo kumi ambazo mtoto huchanjwa kwa awamu tatu tofauti na kuweza kufikia idadi ya chanjo hizo.


Mratibu wa kitengo hicho wilayani hapa, Mary Ngonyani alieleza hayo alipokuwa akihojiwa na mwandishi wetu juu ya maendeleo ya utoaji chanjo kwa watoto wadogo wilayani humo.

“Changamoto kubwa tuliyonayo hapa ni ukosefu wa gari ambalo lingetufanya tuweze kuwafikia walengwa walipo kwa wakati na kufanyia shughuli zilizolengwa  katika kitengo hiki”, alisema.

Ngonyani alisema kuwa wameweza kuvuka lengo hilo la kitaifa, asilimia 95 kwa kufanya kazi kwa ufasaha kutokana na watendaji wachache waliopo kujenga ushirikiano mzuri wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.

No comments: