Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
AGIZO limetolewa kwa Watunza fedha wote waliopo katika
Halmashauri za wilaya hapa nchini, kutimiza wajibu wao wakati wa utekelezaji wa
majukumu yao ya kazi za serikali na kuacha kuwa miungu watu.
Vilevile wametakiwa kuvunja madaraja na minyororo ya ubinafsi,
badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia taratibu husika na maadili ya utumishi
wa umma.
Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo alisema hayo jana alipokuwa
akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
katika ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.
Waziri huyo alisema kuwa katika halmashauri kumekuwa na tabia
kwa baadhi ya Wahasibu kutoa taarifa za uongo kwamba, mfumo wa ulipaji malipo (Epicor)
pale malipo husika yanapotakiwa kufanyika umekuwa ukisumbua jambo ambalo sio la
kweli hivyo wanapaswa kubadilika.
“Wahasibu mmekuwa na ukiritimba wa namna hii, haya yote
yamekuwa yakifanyika kwa lengo la kutengeneza mianya ya rushwa sasa tunataka
mbadilike fanyeni kazi kwa kufuata misingi bora iliyowekwa na serikali kabla
hamjachukuliwa hatua za kinidhamu”, alisisitiza.
Kadhalika amewataka maofisa manunuzi nao wazingatie sheria na
taratibu zilizowekwa katika utendaji wao wa kazi na sio kufanya michakato ya
ugawaji wa tenda kwa njia za upendeleo ili waweze kupewa rushwa.
Wakati huo huo, Jaffo aliongeza kuwa katika halmashauri mpya ya
mji wa Mbinga serikali imetenga shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa
ofisi zake hivyo ameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kukaa na wadau wake
(wananchi) na kufanya majadiliano ambayo yataweka makubaliano mazuri ni wapi
ofisi hizo zijengwe.
Alisema kuwa ni kosa kwa watendaji au viongozi kuketi peke
yao na kufanya maamuzi ambayo hayana maslahi kwa wananchi juu ya ujenzi wa
ofisi hizo ambapo amewataka kuwashirikisha wadau husika ili kuweza kuondoa
malalamiko yasiyokuwa ya lazima kwamba ni eneo gani linafaa kwa ajili ya ujenzi
huo.
No comments:
Post a Comment