Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amesema kwamba amesikitishwa na kitendo cha maofisa Washauri na Wafuatiliaji Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo ambao walipewa dhamana ya kusimamia
zoezi la ugawaji wa fedha kwa kaya maskini, kutotekeleza majukumu yao ipasavyo
na kusababisha fedha hizo kulipwa watu ambao hawakuwa na sifa.
Cosmas Nshenye. |
Aidha alifafanua kuwa kufuatia hali hiyo serikali wilayani
hapa imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Mratibu wa mfuko huo, Ahsante
Luambano ambaye alisema kuwa ameshindwa kuwajibika kwa kusimamia ipasavyo zoezi
la uibuaji wa kaya hizo na kusababisha wengi wao walioingizwa katika mpango wa
kulipwa fedha hizo kuwa ni viongozi wa serikali ngazi ya vijiji na vitongoji.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, Nshenye alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, huku
akiongeza kuwa barua ya Waziri mwenye dhamana ya Desemba 5 mwaka huu ambayo waliipata
imetoa maagizo ya kuwasimamisha kazi waliohusika katika kuvuruga utekelezaji wa
mpango huo kwa muda usiojulikana hadi uchunguzi utakapokamilika na wahusika kuchukuliwa
hatua za kinidhamu.
Nshenye alisema kuwa licha ya kusimamishwa kazi mratibu huyo,
pia hatua za kuwasimamisha watendaji wengine walioshiriki kuhujumu fedha za
mfuko wa TASAF wilayani Mbinga zinafuata na taarifa ya idadi yao kuwa ni
wangapi itatolewa baadaye lengo ikiwa waweze kupisha uchunguzi kufanyika
kuhusiana na jinsi walivyojihusisha kuvuruga utekelezaji wa mfuko huo.
“Kwa mujibu wa utafiti ambao unaendelea kufanyika, hivi sasa
ninataarifa kwamba zaidi ya walengwa hewa 200 waliandikishwa kwenye mpango huu
wa kupewa fedha hapa Mbinga, wengi wao tuna taarifa kwamba ni viongozi wa
serikali ngazi ya vijiji kwa kweli haingii akilini kwa kiongozi wa serikali
kuingizwa kwenye mpango wa kaya maskini wakati anao uwezo wa kumudu maisha yake”,
alisema Nshenye.
Alieleza kuwa endapo watabainika kwa namna moja au nyingine
baada ya uchunguzi unaoendelea kufanyika kwamba wamehusika kuyafanya hayo watachukuliwa
hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi ili iwe fundisho kwa wengine na
jambo hilo lisiweze kujirudia tena.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alisisitiza kuwa
utafiti unaoendelea kufanyika unatekelezwa kwa kupita kaya kwa kaya, ili waweze
kujiridhisha wanufaika hewa jumla yake ni wa ngapi na nani alistahili kupewa
fedha hizo za TASAF.
No comments:
Post a Comment