Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Yakobo
(AJUCO) tawi la Songea mkoani Ruvuma, Henry Mwelang’ombe (24) ambaye ni wa
mwaka kwanza amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia
kamba aina ya manila, kwenye msitu uliopo nyuma ya shule ya sekondari ya
wasichana Songea iliyopo mjini hapa.
Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo,
Zubery Mwombeji alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa na mwalimu mmoja
anayefundisha katika sekondari hiyo ya wasichana ambaye hakutaka kumtaja jina
lake.
Mwombeji alisema kuwa mwalimu huyo alikuwa akielekea shambani
kwake majira ya asubuhi ambapo ghafla aliukuta mwili wa marahemu huyo ukiwa
unaning’inia kwenye mti katika msitu huo Disemba 18 mwaka huu majira hayo ya
asubuhi.
Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma alifafanua kuwa
mwalimu huyo baada ya kuona tukio hilo ambalo lilimshitua, alichukua jukumu la
kutoa taarifa kwa majirani wanaozunguka eneo hilo ambapo baadaye walilazimika
kwenda kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi Songea mjini na askari walikwenda
huko, kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari ambaye alithibitisha
kuwa Henry amefariki dunia kutokana na kujinyonga huko.
Alifafanua kuwa mwili wa mwanafunzi huyo ulikutwa ukiwa
umeharibika vibaya, ambapo inadaiwa kuwa marehemu alikuwa amejinyonga siku
kadhaa zilizopita ambapo waliukuta pia ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye
daftari dogo ambalo lilikuwa na maneno yafutayo;
“Nini maana ya utu, acha nife siwezi kuvumilia, walionitenda
nawaona acha nife tu mimi. Utu sio mavazi marafiki wengi ni wanafiki tulikuwa
safari moja sasa tumetengana, yote sababu ya pesa, fikiria ungekuwa wewe,
nilihisi narekodiwa toka Mbeya sasa ni kweli tuache siasa tubaki kwenye ukweli,
“Nafanya haya sababu sikutaka viungo vyangu vionekane
hadharani, hii ni kwa sababu ya kulinda utu na heshima, ulemavu umekuwa tatizo
kwangu, sikupenda nijione, sitaki nijione mimi ni mkosaji nisamehe Allah”,
ulisema ujumbe huo.
Aidha katika chumba alichokuwa akiishi kulipatikana pia
ujumbe mwingine wa maneno yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili
yaliyosomeka hivi; “My Dream B me true na inauma sana”.
Kadhalika jitihada za mwandishi wa habari hizi kumpata Mkuu
wa chuo cha AJUCO tawi la Songea, Dkt. Longino Lutagwelela ziligonga mwamba
baada ya kuelezwa kwamba yupo Mwanza kikazi lakini mlezi wa chuo hicho Michael
Sinienga alipohojiwa alisema kuwa taarifa za tukio hilo amezipata Disemba 18
mwaka huu majira ya saa tano asubuhi, wakati alipokuwa akitokea kanisani baada
ya kuambiwa na wafanyakazi wenzake.
Sinienga alisema kuwa Henry alikuwa ni mwanachuo wa chuo
hicho mwaka wa kwanza ambapo alikuwa anasomea shahada ya Sanaa na Ualimu na
kwamba taarifa za tukio hilo, tayari ameshaujulisha uongozi wa chuo na taratibu
husika zinatekelezwa za kuusafirisha mwili wake kuelekea Chimala wilayani
Mbarali mkoani Mbeya, nyumbani kwa wazazi wake ambako mazishi yake yanatarajiwa
kufanyika.
Kadhalika alipohojiwa kwamba mwanafunzi huyo inadaiwa kuwa
alikuwa na tatizo la kutopata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo (HESLB), alifafanua
kuwa Marehemu alikuwa miongoni mwa wanafunzi walionufaika na mkopo kutoka
katika bodi hiyo.
Baadhi ya majirani akiwemo mwenye nyumba eneo la Majengo
jirani na eneo la chuo hicho ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao ambako marehemu
katika uhai wake alikuwa amepanga na kuishi huko walieleza kuwa, ni zaidi ya
wiki moja alikuwa hajaonekana pale nyumbani alipokuwa anaishi na kwamba
walikuwa wakihisi kwamba alikuwa chuoni akijisomea pamoja na wanachuo wenzake
kwa kuwa halikuwa jambo geni kwao kutorudi nyumbani kwa sababu ya kujisomea na
wanachuo wenzake.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery
Mwombeji alieleza kuwa kupitia idara yake ya upelelezi makosa ya jinai
uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika kuhusiana na tukio hilo ili kuweza kubaini
chanzo chake na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
No comments:
Post a Comment